Mamia ya raia wa Congo wanaotafuta hifadhi nchini Burundi wamesombwa na maji ya mto Ruzizi wakati wanapokimbia mapigano kati ya M23 na jeshi la Serikali.
Jordan Bita ni mmoja wa raia wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao wanakimbia mapigano kutafuta hifadhi na usalama katika nchi jirani ya Burundi..
Bita sawa na wengine wanalazimika kuogelea umbali ya mita 300, katika mto Ruzizi ambao maji yake yanakwenda kwa kasi sana.
Baada ya kufanikiwa kuvuka mto huu, mizigo ya wanaowasili nchini Burundi inakaguliwa na maafisa wa Burundi na wale ambao hawana chochote ambacho kinaweza kuhatarisha usalama wanaruhusiwa kuingia na kupelekwa hadi kwa kambi ya wakimbizi.
Amani Sebakungu pia anatoka eneo la Kamanyola ambalo kwa sasa linadhibitiwa na waasi wa M23. Pia yeye amelazimika kuvuka mto huu ili kuingia Burundi.
''Mimi sina cha kufanya, ni lazima nivuke mto huu ili niwaletee chakula familia yangu. Ninapokuwa ndani ya mto mimi huwa nimejitolea Maisha yangu. Nikifanikiwa kuvuka sawa, nikilemewa nawaita wenzangu wanisaidie na ikiwa hali itakuwa mbaya bsi ilikuwa siku yangu.'' Alisema Sebakungu.
Kwa waliofanikiwa hatari za kuvuka mto huu zinawaandama hadi katika kambi za wakimbizi.
Mama ambaye hataki jina lake litajwe alimpoteza mtoto wake wa miezi saba baada ya kuugua ugonjwa wa kichomi, uliosababishwa na baridi ya maji ya mto ruzizi.
''Nilipofika mto Ruzizi, siku na la kufanya, niliogelea na mtoto wangu lakini kwa bahati mbaya akanywa maji ya mto Ruzizi na pia maji yalikuwa baridi sana. Hivyo akapata matatizo ya kupumua. Tulimpeleka katika hospitali ya kambi lakini kwa bahati mbaya akafariki. Nasikia uchungu sana'' alisema mama huyu.
Magega Mwarui mwenye umri wa miaka 87 ambaye ana ulemavu wa kuona naye aliogelea mto wakati alipokuwa akikimbia vita vya M23.
Anasema hata kwa sasa hajui ni mara ngapi amevuka mto huu, kwa sababu ameshuhudia msukosuko nchini DRC kwa miaka mingi.
Licha ya kuvuka mto huu, raia hawa wa Congo wanakabiliwa na hatari chungu nzima hasa wakati huu M23 wanapojaribu kuteka maeneo zaidi ya Kivu ya Kusini.
Huku juhudi za jamii ya kimataifa za kutafuta suluhisho la mzozo wa Congo zikiendelea ni matumaini ya Wakongamani kuwa amani itarejea ili nao waweza kurudi nyumbani na kuendelea na maisha yao.
Comments