SERIKALI Imeipongeza Benki ya NMB kwa kuwatambua, kuwajali na kuwathamini Watoto Yatima na Wanaoishi Kwenye Mazingira Magumu kwa namna inavyojitoa kuwafikia, kuona mahitaji na changamoto zao na kushiriki kuzipatia ufumbuzi, kitendo kinachoakisi upendo wa taasisi hiyo kwa wateja wao ambao ndio wazazi na walezi wa watoto hao.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, wakati wa hafla ya futari iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Jumatano ya Machi 5, ambako NMB iliwakutanisha pamoja na kuwafuturisha Wateja wao, Viongozi wa Serikali, Viongozi wa Dini na Watoto Yatima na Wanaoishi kwenye Mazingira Magumu.
Katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, alimkabidhi Waziri Mkuu Majaliwa msaada wa vyakula mbalimbali vitakavyotumika kama futari kwa watoto zaidi ya 239 wanaolelewa na Vituo vya TUYATA (cha Magomeni Mikumi) na Hiyari (cha Mbagala Zakhiem), huku akiweka ahadi ya benki yake kuwahudumia watoto katika kipindi chote cha Ramadhan.
Akizungumza na waalikwa wa hafla hiyo, wakiwemo watoto zaidi ya 100 waliohudhuria, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali imekuwa ikipokea ripoti za mwenendo wa uendeshaji wa maisha ya watoto Yatima kutoka vituo mbalimbali nchini, zinazoonesha uwepo wa changamoto kubwa za kimahitaji, na kwamba NMB inajaribu kuhimiza jamii kuyajali wenye uhitaji.
“Tunaishukuru na kuipongeza Benki ya NMB kwa kutuandalia tukio hili kubwa, lenye kheir na baraka, lililotukutanisha na kufuturu pamoja na Watoto Yatima na Wanaoishi Mazingira Magumu, kitendo hiki ni jambo la kheir, ambalo Mwenyezi Mungu amelihimiza sana kwenye vitabu vyake, pongezi zetu pia kwa walezi wa vituo vya watoto hawa kote nchini.
“Leo hii NMB inapotukutanisha hapa na vijana hawa, maana yake inatuhimiza sisi wengine kuungana na benki hiyo katika kuwatambua watoto hawa, kuona mahitaji yao na kushiriki pamoja katika kuwahudumia, kwani kutoa ni moyo sio utajiri, na kwa maana hiyo chochote ulichonacho waweza kwenda kutoa katika vituo mbalimbali.
“Mlichofanya NMB ni alama ya upendo mlionao kwetu sisi wateja wenu, ambao hawa ni watoto wetu. Pamoja na kwamba tumefungua akaunti kwenye benki yenu, si kwamba tuna uwezo mkubwa, lakini nyie kwa kujali utendaji kazi wenu pamoja na sisi, mmeamua kutumia sehemu ya faida mnayopata, kutambua na kutoa mchango wenu kwa jamii ya wenye uhitaji,” alisema Majaliwa.
Aliongeza ya kwamba NMB imekuwa mfano miongoni mwa taasisi za fedha ambao kila mwaka wanaandaa hafla kama hizo za futari na kuwaalika watoto wadogo Yatima na Wanaoishi Mazingira Magumu kushiriki na baada ya futari na mfungo kumalizika, inawatembelea watoto hawa kwenye maeneo yao kuwauliza shida zao na matamanio yao.
“Leo mnapoungana na wenye vituo hivi kutoa huduma kwa watoto hawa, basi mujue pia kwamba mnaisiadia pakubwa Serikali katika kuhudumia jamii ya wenye uhitaji, kwa hiyo tuwashukuru kwa kuunga mkono jitihada zetu katika kutoa huduma kwa watu wetu. Kwahiyo NMB endeleeni, mambo makubwa mnayoyafanya, tunayaona,” alibainisha Waziri Mkuu.
Kwa upande wake, Bi. Zaipuna alisema imekuwa ni desturi ya NMB kuandaa futari katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, ambako huwaalika wateja, viongozi wa dini na wadau wengine mbalimbali, kuendelea kudumisha ukaribu na kustawisha mahusiano mazuri yaliyopo kati ya benki yake, wateja wao na jamii kwa ujumla.
“Na hakika leo imekuwa ni faraja kubwa kwetu kujumuika na viongozi mbalimbali, wateja wetu wanaotoka hapa Dar es Salaam, na bila kusahau Watoto Yatima na Wanaoishi Kwenye Mazingira Magumu, na huu ni uthibitisho wa dhati wa kaulimbiu yetu ya NMB – Karibu Yako, kwani hata katika nyakati hizi za Kiimani bado benki tunakuwa pamoja na wateja wetu.
“Tutumie mwezi huu kutafakari mazuri yote ambayo Mungu ametujalia na kuendelea kuwa watu wema, wenye kufanya matendo mema katika kipindi hiki cha Ramadhan na hata baada ya mfungo, ambacho ni wakati mzuri kwetu sote kutafakari juu ya maadili yanayotuunganisha binadamu wote - upendo kwa familia zetu, shukrani kwa Mwenyezi Mungu, toba na Ibada Endelevu,” alisema.
“Kwa miaka iliyopita, NMB ilikuwa ikishiriki futari pamoja na watoto wanaotoka kwenye mazingira magumu, iko hivyo pia leo tukiwa tumejumuika pamoja na watoto kutoka vituo vya Tuwalee Yatima Tanzania (TUYATA) cha Magomeni Mikumi na Kituo cha Hiyari kutoka Mbagala Zakheim hapa jijini Dar es Salaam,” aliongeza Bi. Zaipuna.
Alibainisha ya kuwa NMB inaamini kwamba kujumuika na vijana hao ni fursa ya Watoto pia kujifunza na kuendelea kuhamasika katika kutenda mema na kuwa wakarimu kwa watu wengine na kuongeza: “Baada ya futari hii ya leo, NMB tunaahidi kuvisaidia vituo hivi viwili katika kipindi chote cha Mwezi huu mtukufu wa Ramadhan,” alisisitiza.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, CPA David Nchimbi, alimshukuru Waziri Mkuu kwa kutenga muda wa kuhudhuria hafla hiyo, kama walivyofanya viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi wa dini, wateja wao wengine pamoja na watoto kutoka vituo vya TUYATA na Hiyari vya Dar es Salaam.
“Uwepo wenu ndo mafanikio makubwa ya futari hii na ndio ishara ya umoja na ukaribu wetu kama Benki ya NMB, Serikali, jamii inayotuzunguka pamoja na taasisi mbalimbali. Kupitia hafla hii, na Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa ujumla, tunapata wasaa wa kufanya tafakari juu ya huruma, ukarimu na utu mwema,” alisisitiza CPA Nchimbi.
CPA Nchimbi alinukuu moja ya Hadithi za Mtume Muhammad (S.A.W), kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allahu Anhu), anayosema: ‘Wakati mwezi wa Ramadhan unapofika, milango ya Pepo inafunguliwa, milango ya Moto inafungwa, na mashetani hufungwa minyororo,’ na kusema:
“Hivyo, Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni wakati mzuri wa kufanya tafakari juu ya ukuaji wa kiroho, na kujiandaa upya kwa ajili ya mabadiliko chanya. Tutumie fursa hii kutafakari majukumu yetu binafsi na ya pamoja katika kujenga jamii yenye amani na umoja. Tuendelee kuhimiza amani, uelewano na ushirikiano katika maisha yetu ya kila siku.”
Waziri Mkuu Majaliwa (kulia) akiongea na baadhi ya watoto yatima.Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna akizungumza wakati wa hafla hiyo ya futari.

Comments