Timu ya Yanga imeamua kutumia Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kwa michezo yake ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam, Afisa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Yanga, Ally Kamwe, amesema uamuzi huo umetokana na tathmini ya kina iliyofanywa na uongozi wa klabu baada ya droo ya hatua ya makundi kupangwa.
Yanga imepangwa katika Kundi B ikichuana na vigogo wa soka barani Afrika ambao ni Al Ahly ya Misri, AS FAR Rabat ya Morocco na JS Kabylie ya Algeria.
“Kundi hili ni miongoni mwa makundi magumu zaidi. Kwa lugha ya mpira, ni kundi la kifo. Hakuna timu nyepesi, yeyote anaweza kufuzu robo fainali,” amesema Kamwe.
Ameongeza kuwa Klabu ya Yanga tayari imeanza maandalizi kuhakikisha inakuwa miongoni mwa timu mbili zitakazofuzu hatua ya robo fainali.
“Tutaanzia mchezo wa kwanza nyumbani dhidi ya FAR Rabat, kisha tutasafiri kwenda Algeria kucheza na JS Kabylie. Michezo yetu mitatu ya nyumbani tutacheza New Amaan Complex, Zanzibar,” amefafanua Kamwe.
Aidha, amewataka mashabiki wa soka visiwani Zanzibar kujiandaa kuipokea na kuipa sapoti timu hiyo katika safari yake ya kutafuta mafanikio barani Afrika.

Comments