Na Mwandishi Wetu, Mpwapwa
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Dk. Neema Peter Majule, amewataka wanawake nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki nafasi za uongozi na kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi ili kuongeza mchango wao katika maendeleo ya taifa.
Dk. Majule ambaye pia nia Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Dodoma, alitoa kauli hiyo Julai 25, 2026, alipokuwa mgeni rasmi katika tamasha la Mpwapwa Women Gala lililofanyika katika Ukumbi wa CCM wilayani Mpwapwa, mkoani Dodoma.
Alisema wanawake wanapaswa kutumia mazingira wezeshi yaliyopo kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli za uzalishaji na ujasiriamali, huku wakijitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kuongeza idadi ya wanawake katika vyombo vya maamuzi kuanzia ngazi za chini hadi kitaifa.
"Ni wakati wa wanawake kutumia fursa zilizopo kujenga uchumi wao na kushiriki kikamilifu katika uongozi kwa maendeleo ya jamii na taifa," alisema Dk. Majule.
Tamasha hilo liliandaliwa mahsusi kuwatambua na kuwapongeza wanawake kwa mchango wao katika maendeleo ya Wilaya ya Mpwapwa kwa mwaka 2025/2026.
Katika hafla hiyo, wanawake waliofanya vizuri katika sekta mbalimbali walitunukiwa zawadi ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao na kuhamasisha utendaji bora zaidi. Sekta zilizotambuliwa ni pamoja na afya, elimu, kilimo na nyinginezo, ambapo wauguzi, walimu, wakulima na wanawake wengine waliotoa mchango mkubwa walipokea tuzo na zawadi.
Comments