Dkt. Nyansaho ametoa wito huo leo Julai 1,2026 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Serengeti, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kikazi ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, mkoani Mara yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na kusikiliza kero za wananchi.
Akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza, Dkt. Nyansaho amesema amani ndiyo msingi wa maendeleo endelevu, akiwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha nchi inaendelea kuwa tulivu na salama.
“Usalama na amani ya nchi yetu havina chama, havina dini wala havina kabila. Kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi yenye utulivu na umoja,” amesisitiza.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali imepokea na kushughulikia kero mbalimbali zilizowasilishwa na wananchi, ambapo baadhi tayari zimeanza kufanyiwa kazi huku nyingine zikiwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria.
Ameeleza kuwa baadhi ya changamoto hizo zipo katika mchakato wa kisheria mahakamani, hivyo Serikali itaendelea kuheshimu taratibu za haki kwa kuacha taasisi husika kukamilisha majukumu yake kwa kuzingatia sheria na kusikiliza pande zote.
Dkt. Nyansaho ameahidi kufuatilia kwa karibu hoja zote zilizowasilishwa ili kuhakikisha wananchi wanapata majibu sahihi na kwa wakati, huku akisisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mwananchi.
“Tutahakikisha taarifa zote muhimu zinapatikana na zinashughulikiwa ipasavyo ili wananchi wapate suluhisho la kudumu kwa changamoto zao,” amesema.
Sambamba na hayo Dkt. Rhimo Nyansaho, ameipongeza Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza kwa vitendo ahadi zake kwa wananchi wa Serengeti kupitia miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara na maandalizi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Serengeti.
Amesema wananchi wanaendelea kushuhudia matokeo ya uongozi wa Serikali kupitia uboreshaji wa miundombinu inayorahisisha usafiri, biashara na kukuza utalii.
Kadhalika, Amempongeza Waziri Mkuu kwa usimamizi wake wa karibu wa miradi ya maendeleo na kusisitiza kuwa kukamilika kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Serengeti kutafungua fursa mpya za kiuchumi, kuongeza idadi ya watalii na kuchochea maendeleo ya Mkoa wa Mara na Taifa kwa ujumla.
Dkt. Nyansaho ameongeza kuwa wananchi wa Serengeti na Mkoa wa Mara wanaendelea kuiunga mkono Serikali kutokana na utekelezaji wa miradi yenye tija inayoboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa eneo hilo.
ziara ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, mkoani Mara dhamira yake ni kukagua miradi ya maendeleo, kusikiliza kero za wananchi na kutoa maelekezo ya kuboresha huduma mbalimbali za kijamii ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.








Comments