Maisha yana nyakati ambazo mtu anaweza kujihisi amepotea kabisa kama hakuna mwelekeo, hakuna matumaini, na hakuna anayeelewa anachopitia. Ni hisia nzito inayoweza kumfanya mtu ajione hana thamani, kana kwamba njia zote zimefungwa na kesho haina maana tena.
Lakini ukweli wa maisha ni huu: watu wengi tunaowaona leo wakiwa mafanikio makubwa walipitia sehemu hizo hizo za giza. Tofauti yao si kwamba hawakuanguka, bali waliamua kutokaa chini milele. Waligeuza maumivu yao kuwa nguvu ya kusonga mbele, na kila hatua waliyochukua ilijenga hadithi mpya ya maisha yao.
1. Wakati unahisi umepotea, bado ndani yako kuna njia mpya haijagunduliwa
Kuna wakati maisha yanakuwa mazito kiasi cha mtu kuhisi kama amepoteza kila kitu ndoto, matumaini, na hata maana ya kuendelea. Hapo ndipo unajiona kama umefika mwisho, lakini mara nyingi huo ndio mwanzo wa safari mpya isiyoonekana bado.
J.K. Rowling ni mfano mkubwa. Kabla ya Harry Potter hakujua kama kuna siku maisha yake yatabadilika. Alikataliwa mara nyingi, aliishi kwa misaada na alihisi kama ameshindwa kabisa, lakini aliamua kuandika hata akiwa kwenye hali ngumu zaidi. Leo hadithi yake inagusa mamilioni ya watu duniani.
2. Maumivu ya leo yanaweza kuwa msingi wa hadithi yako ya kesho
Maumivu yana uwezo wa kumvunja mtu au kumjenga upya. Watu wengi wanaofanikiwa ni wale waliokubali maumivu yao kama sehemu ya kujifunza, si mwisho wa safari.
Oprah Winfrey alikulia kwenye mazingira magumu sana, akipitia changamoto za ukatili na kukataliwa. Lakini hakuruhusu historia yake imfungie maisha yake. Badala yake, alijenga upya thamani yake na leo ni moja ya wanawake wenye ushawishi mkubwa duniani, akihamasisha mamilioni kila siku.
3. Hata ukianguka mara nyingi, bado unaweza kusimama na kuandika upya maisha yako
Kushindwa si ishara ya mwisho, bali ni sehemu ya mchakato wa mafanikio. Kila anguko linafunza kitu kipya kinachokuandaa kwa hatua inayofuata.
Nelson Mandela alikaa gerezani kwa miaka 27, lakini hakuruhusu kifungo hicho kufuta ndoto zake. Alitoka akiwa na moyo wa msamaha na uongozi, akabadilisha historia ya Afrika Kusini na kuwa ishara ya uvumilivu duniani kote. Anguko lake halikumaliza maisha yake lilimjenga kuwa nguzo ya mabadiliko.
4. Kujihisi umepotea si mwisho ni mwaliko wa kujijenga upya
Kuna wakati mtu hujikuta hajielewi tena, hajui anataka nini, au anaelekea wapi. Huo unaweza kuwa wakati wa hofu kubwa, lakini pia ni nafasi ya kujitafuta upya na kugundua uwezo mpya uliokuwa umefichika.
Steve Jobs alifukuzwa kwenye kampuni yake mwenyewe Apple, jambo lililoweza kumvunja kabisa. Lakini alitumia kipindi hicho kujijenga upya, akarejea baadaye na kubadilisha dunia kupitia uvumbuzi wa teknolojia. Kushindwa kwake hakukuwa mwisho kulikuwa daraja la mafanikio makubwa zaidi.
5. Usikate tamaa ulimwengu haujamaliza kuandika hadithi yako
Kila mtu ana wakati wa giza, lakini pia kila mtu ana nafasi ya mwanga. Kuwa hai leo ni ushahidi kwamba bado kuna ukurasa mpya unaosubiri kuandikwa, hata kama huuoni sasa.
Watu wengi tunaowaona leo kama mfano wa mafanikio walipitia nyakati ambazo walijiuliza kama kuna maana ya kuendelea. Lakini waliendelea hata bila majibu, na baadaye maisha yao yakawa ushuhuda kwamba uvumilivu huzaa matokeo makubwa.
6. Hata pale unapohisi umebakia peke yako, bado kuna nguvu ndani yako hujaigundua
Upweke wa kihisia unaweza kumfanya mtu ajione hana msaada wowote. Lakini mara nyingi, nguvu kubwa ya mtu hujitokeza pale anapokuwa hana mtu wa kumtegemea zaidi yake mwenyewe.
Kuna watu wengi wanaofanikiwa leo waliwahi kupitia vipindi vya upweke mkubwa, lakini walitumia muda huo kujenga nidhamu, ujasiri na malengo mapya. Ndani ya ukimya wao kulikuwa na maandalizi ya ushindi mkubwa.
Maisha yako hayajaisha kwa sababu leo ni ngumu. Badala yake, huenda leo ndio sehemu ya hadithi yako itakayobeba maana kubwa zaidi kesho. Usikubali maumivu ya sasa yafute uwezo wako wa kuwa mtu mkubwa zaidi kuliko unavyofikiria bado hadithi yako inaendelea kuandikwa.
Na Hawa Kashera
Kalamu Ya Mzalendo

Comments