SERIKALI YAWEKA MKAZO UENDELEVU WA HUDUMA ZA VVU, KIFUA KIKUU, MALARIA

 


NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imeweka mkazo katika kuhakikisha huduma za VVU/UKIMWI, Kifua Kikuu (TB) na Malaria zinaendelea kutolewa kwa ufanisi, bila kuathiriwa na mabadiliko ya ufadhili wa nje, huku ikiendelea kuimarisha mifumo ya ndani ya kugharamia na kusimamia huduma hizo ili wananchi kuendelea kupata huduma bora na endelevu.

 

Hayo yameelezwa leo Julai 29,2026 jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Prof. Tumaini Nagu, wakati akifungua Mkutano wa Waganga Wakuu wa Mikoa, Waratibu wa  UKIMWI  wa Mikoa, Waratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma wa Mikoa waratibu wa Huduma za  Maabara, Wafamasia, makatibu wa Afya na Waratibu wa Takwimu.

 

Amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha huduma hizo zinaendelea kutolewa, ikiwemo kutenga Shilingi Bilioni 142 kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vitendanishi na usafirishaji wa sampuli, pamoja na kutenga Shilingi Bilioni 158 katika kila mwaka wa fedha 2025/26 na 2026/27 kwa ajili ya kuendeleza huduma hizo muhimu.

 

"Pamoja na changamoto zilizotokana na mabadiliko ya ufadhili wa nje, Serikali imeendelea kuweka mikakati ya muda mrefu ya kuhakikisha huduma za VVU/UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria zinakuwa endelevu kwa kuimarisha vyanzo vya ndani vya fedha, ikiwemo kuanzishwa kwa Mfuko wa AIDS Trust Fund pamoja na kusaini Mkataba wa Uendelevu wa Huduma hizi kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Marekani," amesema Prof. Nagu.

 

Aidha, Prof. Nagu amewapongeza Makatibu Tawala wa Mikoa, Timu za Usimamizi wa Huduma za Afya za Mikoa (RHMTs) na Halmashauri (CHMTs) kwa kuendelea kujumuisha huduma za VVU, Kifua Kikuu na Malaria katika mfumo wa kawaida wa utoaji wa huduma za afya, hatua ambayo amesema imeongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali zilizopo na kuimarisha uwezo wa mfumo wa afya kukabiliana na mabadiliko ya ufadhili wa nje.

 

Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka OWM-TAMISEMI, Dkt. Rashid  Mfaume, amesema moja ya malengo makuu ya mkutano huo ni kutathmini uendelevu wa utoaji wa huduma za VVU/UKIMWI, Kifua Kikuu, Malaria na huduma nyingine za afya kupitia mifumo ya huduma jumuishi, huku mkazo ukiwa katika kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana yanaendelea kudumishwa kwa upande wa fedha, utekelezaji wa programu na ushirikishwaji wa jamii.

 

Mkutano huo wa siku tatu unawakutanisha viongozi na wataalamu wa sekta ya afya kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara kujadili utekelezaji wa maazimio ya mkutano uliopita, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha huduma jumuishi za VVU/UKIMWI, Kifua Kikuu, Malaria pamoja na huduma nyingine za afya kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma bora, salama na endelevu.






Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

Soma Taarifa ya UTEUZI:Rais Jakaya Kikwete amemteua Dkt. Ben E. Moshi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya PUMA Energy (zamani ilijulikana kama BP Ltd)

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MAAFISA JENERALI WASTAAFU 17 WA JWTZ WAAGWA.

PICHA YA RAIS ILIYOBAMBA WIKI HII

JUA AINA NNE ZA KABILA LA WASUKUMA

18 WAPITISHWA KUGOMBEA UONGOZI YANGA

DK MAGUFULI ATANGAZA KIAMA CHA MAJAMBAZI, WEZI NA MAFISADI KATIKA MIKUTANO YA KAMPENI SUMBAWANGA,TUNDUMA, ILEJE NA MBOZI

BINTI WA KITANZANIA GLORIA MAJULE ASHINDA TUZO YA UANDISHI BORA WA FILAMU YA MALARIA MAREKANI ‎