Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, ametangaza rasmi kuwa Ligi Kuu ya NBC inatarajiwa kuanza kutumia mfumo wa marejeo ya video kuanzia msimu ujao wa 2026/2027. Hata hivyo, badala ya mfumo ghali wa VAR, TFF itashirikiana na FIFA kuleta mfumo rahisi na wa bei nafuu unaojulikana kama Football Video Support (VS) ili kuongeza haki uwanjani.
Tofauti na VAR inayotegemea chumba maalum na waamuzi wengi wa ziada, mfumo huu mpya wa VS utafanya kazi kwa mtindo wa "Changamoto" (Challenge). Makocha wakuu wa timu zote mbili watakuwa na mamlaka ya kuomba mwamuzi wa kati kwenda kurudia kuangalia video kwenye kioo cha pembeni ya uwanja pale wanapoona kuna makosa kwenye matukio makubwa kama magoli, kadi nyekundu, au penalti.
Kila timu itapewa nafasi nne (4) za kuomba marejeo hayo kwa kila mchezo. Kocha akishinda changamoto yake na mwamuzi akabadili maamuzi, idadi ya nafasi zake inabaki pale pale; lakini kama akishindwa na mwamuzi akasimamia msimamo wake wa kwanza, timu inapoteza nafasi moja. Hatua hii inalenga kumaliza malalamiko ya uamuzi huku ikizingatia uhalisia wa kiuchumi wa klabu zetu.
Comments