NA: DK. REUBENI LUMBAGALA
Julai 1, 2026, serikali imeanza utekelezaji wa bajeti mpya kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Yale yaliyopangwa na serikali na kujadiliwa na wabunge na hatimaye yakaafikiwa katika bajeti hiyo, yameanza kufanyiwa kazi ili kufanikisha mipango ya maendeleo.
Wizara ya Fedha kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuja na mabadiliko mbalimbali ya kodi. Mabadiliko haya yamelenga kuleta mageuzi, ufanisi na hatimaye kuongeza mapato bila kumuumiza mlipakodi ambaye ni mdau muhimu katika mipango ya maendeleo.
Kwahiyo, kutokana na mabadiliko hayo, TRA pamoja na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), wameratibu mafunzo kwa wahasibu, wakaguzi, wataalamu wa fedha na washauri wa kodi ili kuwajengea uwezo wa mabadiliko hayo ili ukusanyaji kodi ufanyike kwa ufanisi.
Hivyo basi, baada ya kupata mafunzo hayo, watakuwa na jukumu la kwenda kwa walipakodi na wananchi kuwaelimisha juu ya mabadiliko hayo ili kujenga uelewa wa pamoja ili yale yaliyopangwa yaweze kutimia.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Julai 8, 2026, Jijini Dar es Salaam, Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi, CPA Paul Walalaze, ambaye alimwakilisha Kamishna Mkuu wa TRA, amesema wataalamu hao wanapaswa kunolewa ili kutambua mabadiliko ya sheria za kodi ili kuongeza tija.
"Mafunzo haya yameandaliwa ili kuwajengea uwezo wa kutekeleza vyema majukumu yenu lakini mkawasaidie walipakodi pia ili tija ipatikane," amesema CPA Walalaze.
Katika hatua nyingine, CPA Walalaze amesema, mabadiliko hayo yamehusisha Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Sheria ya Kodi ya Mapato, Sheria ya Ushuru wa Bidhaa na Sheria ya Usajili wa Vyombo vya Moto.
Mabadiliko mengine ni Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sheria ya Ushuru wa Stempu, Sheria ya Uingizaji wa Bidhaa Nchini na Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ikumbukwe kuwa, mkakati wa serikali ni kuhakikisha nchi inajitegemea kibajeti kwa asilimia kubwa kwa kuimarisha ukusanyaji kodi. Tayari, katika bajeti hii ya 2026/2027, asilimia 74.2 ni mapato ya ndani. Jambo hili, linatoa dira ya kufanikiwa mipango ya maendeleo kwani makusanyo ya kodi ndiyo msingi wa kufanikisha mipango hiyo.
Comments