Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake CCM -UWT Taifa Mary Chatanda ametembelea mradi wa ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake UWT Mkoa wa Mbeya wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Mil 80.
Nyumba hiyo ya Katibu wa Jumuiya ya wanawake CCM -UWT imejengwa na Mbunge wa viti Maalumu Mkoa wa Mbeya Mhandisi Maryprisca Winfrid Mahundi kwa ushirikiano wa baadhi ya wadau na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Maryprisca Woman Empowerment Foundation (MWEF).
Akizungumza wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa nyumba hiyo Mheshimiwa Mahundi ambaye pia ni Naibu Waziri Maendeleo ya ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu amesema mradi huo ni sehemu ya miradi mingine iliyopo katika Wilaya za Chunya, Mbarali,Rungwe,Kyela na Mbeya Vijijini inayogharimu zaidi ya Shilingi Mil 150.
Amesema yeye kama Mbunge wa Viti Maalumu amefuata maelekezo yake Mheshimiwa Mwenyekiti UWT Taifa Mary Chatanda ili kuacha athari na alama ya kudumu kwa Jumuiya ya wanawake wa CCM kushiriki ujenzi wa nyumba za viongozi wa UWT.
“Mimi kwa binafsi niliamua kujivisha hili bomu pekee yangu kwa kushirikiana na marafiki zangu na Taasisi yangu ya Maryprisca Woman Empowerment Foundation MWEF,kuacha alama na sadaka yangu kwa Wanawake Mkoa wa Mbeya”amesema Mheshimiwa Mahundi.
Alisema kuwa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Mbeya wamemfanyia jambo kubwa hivyo hiyo kwake ni sehemu ya sadaka na kurejesha shukrani kwa jamii ya wanawake Mkoa wa Mbeya.
“Mama yetu Mary Chatanda hii ni heshima utaiacha kwetu utakumbukwa daima kwa wazo hili endelevu kwa Jumuiya ya Wanawake,umetuheshimisha nasi tunafuata nyayo zako na kutekeleza mawazo yako” amesema Mheshimiwa Mahundi.
Akipokea taarifa hiyo Mwenyekiti wa Jumuiya wa Wanawake Taifa Mheshimiwa Mary Chatanda amesema kwa upande amemshukuru Mheshimiwa Maryprisca Winfrid Mahundi kwa kujitoa kwake kwa hali na mali kukamilisha mradi huo jambo ambalo linakipa moyo Chama kuendelea kuunga mkono jitihada zake.
“Tunakupongeza sana kwa moyo wako uliouonesha kwa Chama chetu, Mimi binafsi nakupongeza sana,Mnyonge Mnyongeni haki yake mpeni, umetoa sadaka sisi tunaipokea kwa mikono miwili,hongera sana.”amesema Mheshimiwa Chatanda.
Aidha Mheshimiwa Chatanda amesema kwa kuonesha namna ambavyo ameridhishwa na kufurahishwa UWT Taifa itamuandikia barua maalumu ya kumshukuru Mheshimiwa Maryprisca ili kuendelea kumtia moyo.
Mheshimiwa Mary Chatanda yupo mkoani Mbeya kwa ziara maalumu ya kutembelea miradi mbalimbali ya Jumuiya hiyo.











Comments