NA MWANDISHI WETU
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Gifted Nature NGO, limejipanga kuwezesha na kutengeneza fursa kwa jamii hususan vijana ili kuwainua kiuchumi na maisha yenye tija endelevu.
Dkt Sophia Kizigo, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa leo, amebainisha kwamba wanakusudia kufikia dhamira hiyo kupitia wa Shujaa Path.
Amesema mradi huo, ulioanzishwa mwaka 2025 kwa lengo la kuwawezesha wavulana na vijana wa kiume ambao mara nyingi hawapati uangalizi wa kutosha katika programu mbalimbali za maendeleo.
Pia ameongeza kwamba kupitia programu mbalimbali zinazolenga jamii, wanajikita kukabiliana na changamoto za kijamii na kimazingira huku likihamasisha elimu, uongozi, ukuzaji wa ujuzi, uwajibikaji na ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo.
"Mradi huu umeanzishwa kutokana na changamoto zinazowakabili wavulana, ikiwemo kuacha shule au kutoshiriki kikamilifu katika elimu.
Pia limeanzishwa kutokana na uwepo wa ukosefu wa malezi na ushauri wa kitaalamu, ajira na fursa za kiuchumi, pamoja na ushawishi hasi wa rika na ukosefu wa mazingira bora ya kukuza vipaji na uwezo wao", amesemaa
Aidha amesisitiza kupitia kaulimbiu “Every Boy, A Shujaa – Kila Kijana wa Kiume ni Shujaa,”
Hivyo Shujaa Path inalenga kuwasaidia vijana kutambua thamani na uwezo wao, kujenga kujiamini, kuwa na maadili mema na kupata ujuzi wa maisha, ujasiriamali na ajira.
Pia amefafanua kuwa, mpango huo unalenga kuwaandaa vijana wa kiume kuwa viongozi na raia wenye mchango chanya katika familia na jamii zao, huku ukiweka mkazo katika kujenga mazingira yatakayowawezesha kutumia vipaji na uwezo wao kwa manufaa yao na jamii kwa ujumla.
"Gifted Nature NGO inaamini kuwa kumjenga kijana leo ni kuijenga jamii bora ya kesho. Kwa kushirikiana na Serikali, shule, jamii, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na vyombo vya habari, shirika hili tutawafikia wavulana na vijana wengi zaidi Tanzania" amesema.

Comments