Dar es Salaam-Tanzania, 07 Agosti 2026: Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) imeendelea kuthibitisha ubora wa bidhaa zake katika jukwaa la kimataifa baada ya kutunukiwa Gold Quality Awards kutoka taasisi ya kimataifa ya Monde Selection, kupitia bidhaa zake za Serengeti Lite, Serengeti Lager, Serengeti Lemon pamoja na TZee.
Tuzo hizi zinatolewa kwa bidhaa zinazokidhi viwango vya juu vya ubora
duniani baada ya kufanyiwa tathmini ya kina na jopo huru la wataalamu wa
kimataifa. Bidhaa hupimwa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo ubora wa
bidhaa, ladha, mwonekano, ubunifu, taarifa kwa watumiaji pamoja na uzoefu wa
matumizi, kwa lengo la kuhakikisha zinakidhi viwango vya kimataifa vya ubora.
Monde Selection ni taasisi ya kimataifa ya kutathmini ubora wa bidhaa za
walaji iliyoanzishwa mwaka 1961 jijini Brussels, Belgium. Kwa zaidi ya miaka
65, taasisi hiyo imekuwa ikifanya tathmini za kitaalamu kwa maelfu ya bidhaa katika
makundi mbalimbali ikiwemo vyakula, bia, vinywaji, vileo, bidhaa za afya na
lishe pamoja na vipodozi. Tathmini hizo hufanywa na zaidi ya wataalamu 80 wa
kimataifa, huku bidhaa kutoka takribani nchi 150 zikiwa zimewahi kufanyiwa
tathmini na kutambuliwa kwa ubora wake.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Mkurugenzi wa Ugavi wa
SBL Joseph Cheloti, alisema ushindi huo
ni uthibitisho wa juhudi za kampuni katika kuhakikisha kila bidhaa inayowafikia
watumiaji inazingatia viwango vya juu vya ubora.
"Kupokea Gold Quality Awards kutoka Monde Selection ni heshima
kubwa kwetu na uthibitisho kuwa bidhaa zetu zinakidhi viwango vinavyotambulika
kimataifa. Tunajivunia mafanikio haya ambayo yanatokana na kujitolea kwa
wafanyakazi wetu, ubora wa malighafi tunazotumia pamoja na mifumo yetu ya
uzalishaji. Zaidi ya yote, tunawashukuru wateja wetu kwa kuendelea kutuamini na
kutuchagua kila siku."
Aliongeza kuwa kampuni itaendelea kuwekeza katika ubora, ubunifu na
maendeleo ya bidhaa zake ili kuhakikisha Watanzania na watumiaji katika masoko
mengine wanaendelea kupata bidhaa zenye viwango bora vinavyotambulika duniani.
Kutunukiwa kwa bidhaa nne kwa wakati mmoja kunaiweka Serengeti Breweries
Limited miongoni mwa wazalishaji wanaoendelea kuonesha ushindani katika sekta
ya vinywaji kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyotambulika kimataifa, huku
ikiendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania katika soko la dunia.
Kuhusu
Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL)
Kampuni ya Bia ya
Serengeti (SBL) ni moja ya kampuni zinazoongoza katika sekta ya vinywaji nchini
Tanzania na ni sehemu ya Diageo PLC, kampuni inayoongoza duniani katika
biashara ya vinywaji. Kampuni inazalisha na kusambaza bidhaa mbalimbali
zinazopendwa na Watanzania ikiwemo Serengeti Premium Lager, Serengeti Lite,
Serengeti Lemon, Pilsner Lager, Guinness, Senator, Kibo Gold, Smirnoff Ice,
Johnnie Walker, Bailey's pamoja na TZee.
SBL inaendelea
kuwekeza katika ubora wa bidhaa, maendeleo ya jamii, uhifadhi wa mazingira,
kilimo endelevu na ukuaji wa uchumi wa Tanzania kupitia shughuli zake za
biashara na ushirikiano na wadau mbalimbali.
Kuhusu
Monde Selection
Monde Selection ni
taasisi huru ya kimataifa inayobobea katika kutathmini ubora wa bidhaa za
walaji, iliyoanzishwa mwaka 1961 jijini Brussels, Belgium. Kwa zaidi ya miongo
sita, taasisi hiyo imekuwa ikitambua bidhaa zinazokidhi viwango vya juu vya
ubora kupitia World Quality Awards, zinazotolewa baada ya tathmini ya kina
inayofanywa na jopo la wataalamu wa kimataifa.
Katika kipindi cha
miaka mitatu iliyopita, zaidi ya bidhaa 9,000 kutoka duniani kote zimefanyiwa
tathmini na majopo ya Monde Selection. Kila mwaka, zaidi ya wataalamu 80 kutoka
fani mbalimbali, wakiwemo wataalamu wa ladha, ubora wa bidhaa, lishe, kemia,
uhandisi wa chakula na afya, hushiriki katika mchakato wa kupima na kutathmini
bidhaa kwa kutumia viwango vya kisayansi na kitaalamu.
Tuzo za Gold Quality
Award hutolewa kwa bidhaa zinazofikia viwango vya juu vya ubora baada ya
kupitia mchakato huo wa tathmini. Leo, alama ya Monde Selection inatambulika
duniani kama ishara ya ubora, uaminifu na uthibitisho wa viwango vya kimataifa
vya bidhaa.
Kwa Mawasiliano Zaidi
wasiliana na:
Comments