Na WMA- DODOMA.
Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa Wakala wa Vipimo (WMA), Bw. Francis Olwero amewapongeza watumishi wa Wakala wanaotoa elimu ya vipimo katika Maonesho ya Wakulima, Mifugo na Uvuvi (Nane Nane) yanayofanyika kitaifa Viwanja vya John Samwel Malecela, Dodoma.
Akishiriki Ufunguzi rasmi wa Maonesho hayo, Agosti 01, 2026, Mkurugenzi Olwero alifurahishwa na jinsi watumishi wanavyotoa elimu na huduma kwa wakulima, wafugaji na wavuvi wanaotembelea maonesho hayo.
“Napenda niwapongeze sana kwa kazi nzuri mnayofanya. Hii ndiyo WMA tunayotaka – kuwa karibu na mwananchi na kutoa elimu inayogusa maisha yake moja kwa moja,” alisema Mkurugenzi.
Aliongeza kuwa elimu ya vipimo inayotolewa na timu ya WMA ni silaha muhimu ya kulinda wakulima dhidi ya hasara. Alisisitiza kuwa kila mkulima anayetoka kwenye banda la WMA akielewa jinsi ya kutumia na kudai kipimo sahihi, “basi tunakuwa tumefanikiwa kutekeleza dhamira yetu.”
Kwa upande wao watumishi walishukuru kwa pongezi hizo na kuahidi kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa siku zilizobaki za maonesho. Walisema wako tayari kuhakikisha kaulimbiu ya *”Pima kwa Usahihi, Pata Faida Halali”* inafika kwa kila mdau wa kilimo, mifugo na uvuvi aliyetembelea Nane Nane 2026.
Aidha, walisema lengo lao ni kuoanisha kaulimbiu hiyo iendane kwa vitendo na kaulimbiu ya Taifa ya NaneNane kwa mwaka 2026 isemayo *”Tambua Soko, Ongeza Tija Kutekeleza DIRA 2050.”*
Mkurugenzi Olwero pia alitembelea Banda la Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara na kuwapongeza kwa ushiriki wenye tija.




Comments