WAKALA WA VIPIMO WAELEZA TIBA YA GESI PUNGUFU

 WANANCHI  wametakiwa kuhakikisha wanapima mitungi ya gesi kabla ya kuinunua ili kujiridhisha kuwa wanapata kipimo cha gesi kinacholingana na fedha wanazolipa, huku wafanyabiashara wote wa gesi wakikumbushwa kutimiza matakwa ya kisheria ya kuwa na mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo (WMA).

Rai hiyo imetolewa na Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Singida, Willie Amosi, wakati wa Maonesho ya 49 ya Kilimo ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma ambapo amesema matumizi ya gesi ya kupikia yameongezeka kwa kasi kufuatia jitihada za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

Amesema jukumu la Wakala wa Vipimo ni kuhakikisha kila mtungi wa gesi unaouzwa kwa wananchi unakuwa na kipimo sahihi cha gesi kama kilivyoainishwa na mzalishaji, ili kumlinda mlaji dhidi ya hasara inayoweza kusababishwa na vipimo visivyo sahihi.

“Wananchi wana haki ya kujiridhisha kuwa gesi wanayonunua ina uzito sahihi. Ndiyo maana sheria inamtaka muuzaji wa mwisho kuwa na mizani iliyohakikiwa na WMA ili kila mnunuzi aweze kupima mtungi wake kabla ya kuuchukua,” amesema Amosi.

Ameeleza kuwa kila mtungi wa gesi hubeba taarifa zinazoonyesha uzito wa mtungi wenyewe pamoja na kipimo cha gesi kilichomo ndani, hivyo mnunuzi anapaswa kulinganisha taarifa hizo kwa kupima mtungi kwenye mizani iliyothibitishwa.

Amosi amesema WMA inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa wazalishaji, wafungashaji na wauzaji wa gesi nchini ili kuhakikisha vipimo sahihi vinazingatiwa, huku akibainisha kuwa malalamiko kuhusu upungufu wa gesi katika mitungi ya matumizi ya majumbani yamepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na kuimarika kwa usimamizi.

Hata hivyo, amewataka wananchi kutoridhika na kupokea mitungi bila kupimwa, akisema ushiriki wao katika kuhakiki uzito wa gesi ni njia muhimu ya kulinda haki zao kama walaji na kuchangia uwajibikaji kwa wafanyabiashara.

Aidha, amewatahadharisha wauzaji wa gesi ambao hawana mizani inayotakiwa kisheria kuhakikisha wanaipata haraka, akisisitiza kuwa ukaguzi wa WMA unaendelea nchini kote na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa watakaobainika kukiuka sheria.

Ametoa wito kwa wananchi wanaotembelea Maonesho ya Nane Nane kutembelea banda la Wakala wa Vipimo ili kupata elimu kuhusu haki zao katika ununuzi wa gesi na bidhaa nyingine zinazouzwa kwa kutumia vipimo, akisisitiza kuwa usahihi wa vipimo ni msingi wa biashara ya haki na ulinzi wa maslahi ya mlaji.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

Soma Taarifa ya UTEUZI:Rais Jakaya Kikwete amemteua Dkt. Ben E. Moshi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya PUMA Energy (zamani ilijulikana kama BP Ltd)

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MAAFISA JENERALI WASTAAFU 17 WA JWTZ WAAGWA.

JUA AINA NNE ZA KABILA LA WASUKUMA

BINTI WA KITANZANIA GLORIA MAJULE ASHINDA TUZO YA UANDISHI BORA WA FILAMU YA MALARIA MAREKANI ‎

HII NDIYO CV YA KOCHA MPYA WA YANGA

KOCHA WA MC ALGERS AIHOFIA YANGA

PICHA YA RAIS ILIYOBAMBA WIKI HII

CDF MKUNDA AWATAKA MAAFISA JENERALI WASTAAFU KUACHA KUHANGAIKA NA SIASA