TANESCO YAENDELEA KUIMARISHA MIUNDOMBINU KUKABILIANA NA MVUA ZA EL NIÑO


NA  MWANDISHI WETU


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) leo Septemba 22, 206 limeendelea na kampeni yake ya kuelimisha umma kuhusu matumizi ya umeme salama wakati wa elnino sambamba na kueleza mikakati inayoendelea kuchukuliwa katika kuimarisha miundombinu ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua za El Niño.


Hatua hizo ni pamoja na kukagua miundombinu, kubaini na kutatua changamoto, pamoja na kutathmini maeneo yanayoweza kuathiriwa na mafuriko au maporomoko ya ardhi ili kuweka uthabiti wa miundombinu ya umeme.


Akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na TBC, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja TANESCO,  Irene Gowelle, amesema TANESCO imejizatiti kuhakikisha huduma ya umeme inaendelea kuwepo kwa usalama endapo mvua hizo zitanyesha.


“Wananchi wanaweza kututaarifu TANESCO kama kuna mazingira yanayowazunguka ambayo kuna nguzo imeanguka imeoza au kuinama na Wanaweza kutupigia picha na kututumia kupitia kurasa zetu za kijamii, makundi yetu ya WhatsApp au kupiga simu kupitia namba 180 ili tuweze kufika na kurekebisha mapema kabla madhara hayajatokea,” amesema Bi. Gowelle.


Naye Meneja Afya na Usalama TANESCO,  Fred Kayega, amesema maandalizi ya mapema ni muhimu katika kuzuia madhara yanayoweza kusababishwa na umeme wakati wa mvua.


Amesisitiza wananchi kutoa taarifa mapema wanapoona miti imeanguka kwenye miundombinu ya umeme au hali nyingine inayoweza kuhatarisha usalama wa watu na miundombinu.


Katika mahojiano kupitia kipindi cha Kumekucha kinachorushwa na ITV, Meneja wa Mawasiliano TANESCO, Agustino Kasale, amesema TANESCO pia imejipanga kuhakikisha mabwawa yanayotumika kuzalisha umeme yanaendelea kudhibitiwa wakati wa ongezeko la maji.


Amesema mabwawa hayo yamejengwa kwa kuzingatia viwango tofauti vya maji na yana vifaa maalumu vya kufuatilia kiwango cha maji.


“Endapo maji yatafikia kiwango cha mwisho, utaratibu wa kuyaachia maji hufanyika na kuwashirikisha wananchi wanaoishi maeneo ya karibu na mabwawa ili kuchukua tahadhari mapema,” amesema Kasale.


TANESCO imewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kupitia namba 180 au njia nyingine rasmi za mawasiliano pale wanapoona hali inayoweza kuhatarisha usalama wa umeme, ili hatua zichukuliwe kwa wakati.




Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MATUKIO MBALIMBALI WAKATI WA KUAPISHWA NDEJEMBI KUWA MAKAMU WA RAIS

𝐌𝐉𝐔𝐄 𝐊𝐀𝐂𝐇𝐄𝐑𝐎 𝐌𝐙𝐄𝐍𝐀

URUSI, CHINA, IRANI NA KOREA KASKAZINI WAPANGA KUUNDA JESHI MOJA LA KUJIHAMI

MAFAO YA MAKAMU WA RAIS ALIYEJIUZULU

KATIKA MWAMBA HUU NITALIJENGA KANISA.

PANYA MAGAWA WA SUA TANZANIA AJENGEWA MNARA WA HESHIMA CAMBODIA