Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amesema wanawake viongozi wa ukanda wa nchi za maziwa makuu ni chachu ya maendeleo kwani, mchango wao umeendelea kuonekana ndani na nje ya nchi zao na duniani kwa ujumla hivyo, ni muhimu kuendelea kuwekeza katika kizazi kijacho cha wanawake viongozi.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo Septemba 18, 2026, jijini Dar es Salaam, kwenye hafla iliyofunguliwa na Mhe. Daniel Baran Silo (Mb), Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuutangazia umma kuhusu ujio wa Mkutano wa Wabunge Wanawake wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (FP-ICGLR), unaotarajiwa kufanyika Novemba 2–5, 2026, jijini Dar es Salaam na kuwa Mgeni Rasmi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akitoa salaam zake, Dkt. Gwajima, alibainisha na kuwapongeza viongozi wanawake mbalimbali nchini Tanzania ambao, wameandika historia kubwa ya mchango kwenye maendeleo ya Taifa, Afrika na dunia kwa ujumla.
Dkt. Gwajima amesema, mkutano huo utakutanisha nchi 12 za Ukanda wa Maziwa Makuu na utajadili masuala mbalimbali yanayohusu amani, ulinzi, usalama na maendeleo, pamoja na nafasi ya wanawake katika uongozi na ujenzi wa amani.
Aidha, amesema, kufanyika kwa mkutano huo nchini Tanzania ni heshima kubwa ya kutambua mchango wa Tanzania kwenye ajenda ya wanawake, Amani na usalama na inatoa fursa muhimu kwa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu kubadilishana uzoefu kuhusu namna Mabunge yanavyoweza kutumia nafasi zao kuhakikisha wanawake wanashirikishwa na kuwezeshwa katika mipango, bajeti na mifumo ya kitaifa ya uwajibikaji.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (FP-ICGLR), Mhe. Balozi Dkt. Deo Mwapinga, amesema, Tanzania ni chimbuko la mipango mbalimbali ya amani na usalama katika eneo hilo akirejea Azimio la Dar es Salaam la mwaka 2004, lililoweka msingi muhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kushughulikia masuala ya amani, usalama na maendeleo.
Aidha, Dkt. Mwapinga ameongeza kuwa, Tanzania inakumbukwa barani Afrika kwa nafasi yake katika harakati za ukombozi wa sehemu kubwa ya Afrika, ikiwa mwenyeji wa Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afrika (Southern Africa Liberation Committee), pamoja na mchango wake katika juhudi za kujenga bara lenye umoja, amani na ustawi.
Comments