NA THADEI HAFIGWA, MOROGORO
JITIHADA za kuimarisha huduma za kijamii, kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kuinua uchumi wa wakulima ni miongoni mwa masuala muhimu yanayoamua kasi ya maendeleo ya Jimbo la Malinyi, mkoani Morogoro.
Chini ya uwakilishi wa Mbunge wa jimbo hilo, Dkt. Mecktridis Fratern Mdaku, masuala ya maji, barabara, kilimo, umwagiliaji na athari za mafuriko yameendelea kuwasilishwa serikalini kupitia mijadala ya Bunge na hoja zinazolenga kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi.
Katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2026/2027, mbunge huyo alieleza kuwa zaidi ya Shilingi bilioni 1.1 zinatarajiwa kutekeleza miradi ya maji katika maeneo ya Malinyi, Ihowanja, Biro, Misegese, Mbalinyi na Kilosa Mpepo.
Alieleza pia kuwa baadhi ya miradi hiyo ilikuwa imekwama na kwamba utekelezaji wake unatarajiwa kusaidia kupunguza adha ya maji kwa wananchi.alitaja changamoto za uchakavu wa miradi ya maji ya Mtimbira na Itete.
Kwa mujibu wa maelezo yake bungeni, mradi wa Mtimbira uliojengwa miaka ya 1980 uliokuwa ukihudumia watu takribani 12,000, sasa unahudumia watu wapatao 72,000, jambo linaloonyesha ongezeko la mahitaji ya huduma hiyo.
Aliziomba mamlaka husika kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa matenki, mabomba na miundombinu mingine.
Pia, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma ya maji katika maeneo ya Madega, Njasa, Lumbanga, Mkanga, Butu na Shinyanga, ikiwemo uwezekano wa kuchimba visima virefu.
Hoja hizi zinaonyesha kuwa suala la maji limepewa nafasi katika uwakilishi wake wa kibunge. Hata hivyo, ili wananchi waweze kutathmini mafanikio kwa usahihi, ni muhimu kuweka wazi kiasi cha fedha kilichopokelewa na kutumika, hatua iliyofikiwa katika kila mradi na idadi ya kaya zinazopata maji baada ya utekelezaji.
Kwa jimbo ambalo shughuli za kilimo ni mhimili wa maisha ya wananchi wengi, barabara ni nyenzo muhimu katika kusafirisha mazao, kupunguza gharama za usafiri na kuunganisha wakulima na masoko.
Dkt. Mdaku aliwasilisha hoja kuhusu uharibifu wa barabara uliotokana na unaosababishwa nyakati za mvua kubwa na mafuriko. Alisisitiza umuhimu wa kujenga miundombinu inayoweza kuhimili hali hiyo ya mazingira.
Alitaja umuhimu wa kuharakisha ujenzi wa barabara ya Kuroka–Ifakara–Lupilo–Mtimbira, kuboresha barabara ya Malinyi-Lumbecha-Londo-Namtumbo, pamoja na kuzingatia daraja la Mto Fulwa na kivuko cha Kikove.
Hoja nyingine muhimu ni ujenzi wa barabara ya Ifakara-Lupilo hadi Malinyi kwa kiwango cha lami.
Aidha,katika majibu ya serikali bungeni Aprili 2026, ilielezwa kuwa ujenzi wa barabara ya Ifakara-Lupilo-Mtimbira yenye urefu wa kilomita 112 ulikuwa umefikia hatua ya kusainiwa kwa mkataba, huku taratibu za malipo ya awali kwa mkandarasi zikiendelea. Serikali pia ilisema sehemu zilizobaki zingehitaji upatikanaji wa fedha.
Kwa hiyo, kipimo muhimu cha mafanikio katika eneo hili kitakuwa kasi ya kazi, ubora wa barabara, upatikanaji wa vivuko na madaraja salama, pamoja na uwezo wa wananchi kusafirisha mazao katika misimu yote ya mwaka.
Katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Dkt. Mdaku alisisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu ya kilimo na upatikanaji wa ardhi kwa wakulima wadogo na wa kati.
Ni wazi kuwa kilimo ni nguzo muhimu ya uchumi wa wananchi wa Malinyi, hivyo, mafanikio ya uongozi unapaswa kupimwa kwa namna wakulima wanavyopata ardhi, pembejeo, maji ya umwagiliaji, masoko na malipo ya mazao yao.
Alipongeza kuanzishwa kwa mradi wa umwagiliaji katika Kata ya Itete, lakini akaeleza kuwa mradi huo unakabiliwa na changamoto za barabara za kufika mashambani na mifereji isiyokidhi mahitaji.
Pia, alikumbushia miradi ya umwagiliaji ya Usangule, Sofi na Mtakasisi, akitaka kuwepo kwa ratiba ya utekelezaji na fedha za kuanzisha kazi.,kwa mantiki kwamba masuala haya yanaonyesha kuwa uwekezaji wa umwagiliaji haupaswi kuishia kwenye ujenzi wa mifereji pekee. Unahitaji pia barabara za mashambani, usimamizi wa matumizi ya maji, upatikanaji wa teknolojia na elimu ya kilimo cha kisasa.
Hoja nyingine ambayo Dkt. Mdaku pia alizungumzia mfumo wa Stakabadhi Ghalani na changamoto zinazowakabili wakulima, ikiwemo ucheleweshaji wa malipo.Alitaja kuwepo kwa vyama 22 vya ushirika vya AMCOS katika jimbo hilo na kueleza umuhimu wa kuwa na mfumo unaohakikisha wakulima wanalipwa kwa wakati.

Comments