LAAC YAWEKA KITIMOTO HALMASHAURI TATU NJOMBE
Yataka majibu ya hoja za CAG, yasimamia mapato, madeni na mikopo ya makundi maalumu
NJOMBE: Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeweka kitimoto katika Halmashauri tatu za Mkoa wa Njombe, ikiwataka watendaji wake kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali za ukaguzi zilizobainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka ya fedha 2023/2024 na 2024/2025.
Kamati hiyo imekutana na watendaji wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, Halmashauri ya Mji wa Njombe na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, ikiwa ni sehemu ya jukumu lake la kuchunguza matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha hoja za ukaguzi zinapatiwa ufumbuzi.
Kikao hicho kiliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Abdallah Dadi, ambaye alisimamia majadiliano na watendaji wa halmashauri hizo kuhusu hoja zilizotokana na ukaguzi wa hesabu za serikali za mitaa.
Akielezea maeneo yanayopewa kipaumbele na kamati hiyo, Chikota amesema LAAC inafuatilia kwa karibu mwenendo wa ulipaji wa madeni kwa kuzingatia umri wa madeni hayo, hatua inayolenga kupunguza malalamiko na kuhakikisha halmashauri zinatekeleza wajibu wake kwa wakati.
Amesema kamati hiyo pia inachunguza mwenendo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani, utoaji wa mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri husika.
Maeneo hayo ni muhimu katika kuhakikisha fedha za umma zinakusanywa na kutumika kwa mujibu wa sheria, huku wananchi wakipata huduma bora na kunufaika na miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.
Katika kikao hicho, watendaji wa halmashauri hizo, wakiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, akiwemo viongozi wa halmashauri, wakurugenzi na maofisa wengine, wanatakiwa kujibu hoja zinazowasilishwa na wajumbe wa kamati kwa uwazi, usahihi na kwa kuzingatia ushahidi wa nyaraka za kiutendaji na kifedha.
Kamati hiyo, ambayo inatekeleza majukumu yake kwa niaba ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ina wajibu wa kuisimamia Serikali katika matumizi ya rasilimali za umma ili kuhakikisha uwajibikaji, nidhamu ya matumizi ya fedha na utekelezaji wa majukumu kwa maslahi ya wananchi.
Uchunguzi wa hoja za ukaguzi ni miongoni mwa hatua muhimu za kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, kubaini mapungufu katika mifumo ya kiutendaji na kuhakikisha kasoro zinazoainishwa zinapatiwa ufumbuzi unaostahili.
Comments