NA MWANDISHI WETU, MANYARA
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Wizara ya Madini kwa usimamizi mzuri wa shughuli za uchimbaji wa madini ndani ya Ukuta wa Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, huku ikitaka kuimarishwa kwa tafiti za madini ili kuongeza fursa za uwekezaji, ajira na manufaa ya rasilimali hizo kwa wananchi.
Akizungumza leo, Oktoba 24, 2026, baada ya kukamilika kwa ziara ya Kamati hiyo katika eneo la Ukuta wa Mirerani, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Subira Mgalu, amesema wananchi wameendelea kunufaika na mnyororo wa thamani wa madini kupitia shughuli za uchimbaji, uongezaji thamani, biashara ya madini na utoaji wa huduma mbalimbali kwa wadau wa sekta hiyo.
Katika ziara hiyo, Kamati pia imetembelea migodi ya madini ya Franone Mining and Gem Co. Ltd na Chusa Mining Co. Limited, pamoja na Kituo cha Biashara ya Madini ya Tanzanite, kwa lengo la kujionea shughuli za uchimbaji, biashara na uongezaji thamani wa madini, pamoja na kutathmini hatua zinazochukuliwa kuimarisha usimamizi wa rasilimali hizo.
Mgalu ameitaka Wizara ya Madini, kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), kuimarisha tafiti katika maeneo mbalimbali yenye rasilimali za madini na kutangaza fursa zilizopo ili kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta hiyo.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuwawezesha wachimbaji wadogo kukuza shughuli zao na kuingia katika uchimbaji wa kati na mkubwa, kuongeza uzalishaji na ajira, pamoja na kuimarisha mchango wa sekta ya madini katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
“Tunataka siku za usoni kuzalisha mabilionea katika Sekta ya Madini kutoka miongoni mwa wachimbaji wadogo, ambao watakuwa wachimbaji wa kati na wakubwa, na hivyo kuzalisha ajira zaidi na kuongeza mchango wa sekta hii katika ukuaji wa uchumi wa nchi,” amesisitiza Mhe. Mgalu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, amesema Serikali kupitia Wizara ya Madini imetenga fedha kwa ajili ya utafiti wa madini, hatua inayolenga kuwawezesha wachimbaji wadogo kuendesha shughuli zao kwa uhakika zaidi na kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, wadau wa madini katika eneo la Mirerani wameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa juhudi za kutatua changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za kila siku.
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Manyara, Tawi la Mirerani, Samwel Rugemalila, ameishukuru Serikali kwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa kuboresha sekta hiyo.
Hata hivyo, ameiomba Serikali kuendelea kuboresha huduma muhimu, ikiwemo upatikanaji wa umeme na maji, ili kuongeza ufanisi na uzalishaji katika shughuli za uchimbaji.
Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Madini ndani ya Ukuta wa Mirerani, Magreth Nelson, ameishukuru Serikali kwa kurejesha mnada wa madini, akisema hatua hiyo imewawezesha wafanyabiashara kuuza madini yao kwa uwazi na katika mazingira ya ushindani wa bei.
Akielezea hali ya uzalishaji wa madini ya Tanzanite, Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Mirerani, George Kaseza, amesema kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, kuanzia Julai hadi Septemba 2026, jumla ya gramu 274,634.32 za Tanzanite zilizalishwa, zikiwa na thamani ya shilingi bilioni 3.23. Aidha, uzalishaji wa Tanzanite Beads ulikuwa gramu 8,622,049.36 zenye thamani ya shilingi milioni 95.83, huku Tanzanite Clive ikiwa na uzito wa gramu 20,562.35 na thamani ya shilingi milioni 16.73.
Amesema Serikali imeendelea kuimarisha ukaguzi na udhibiti wa utoroshaji wa Tanzanite kupitia hatua mbalimbali, ikiwemo kuanzishwa kwa Cheti cha Uasilia wa Madini ya Tanzanite mwaka 2010, ujenzi wa Ukuta wa Mirerani uliokamilika Aprili 2018 na kuanzishwa kwa Soko la Madini Mirerani mwaka 2021. Aidha, eneo hilo lina kamera za usalama (CCTV) 310 na taa 573, huku mwaka 2026 Serikali ikiagiza kofia ngumu 12 zenye kamera kwa ajili ya wadhibiti wa madini chini ya migodi. Kamera hizo husaidia kurekodi hatua za uzalishaji hadi madini yanapofungiwa lakiri ya Serikali na kufikishwa juu ya ardhi, hatua inayolenga kuongeza uwazi na kuzuia utoroshaji.
Kuhusu biashara ya Tanzanite, Kaseza amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, mnada wa wafanyabiashara wadogo uliofanyika Mei 15, 2026, uliwezesha kuuzwa kwa gramu 2,809.31 za Tanzanite zenye thamani ya shilingi 271,270,100, huku mnada wa wafanyabiashara wakubwa uliofanyika Mei 21, 2026, ukiwezesha kuuzwa kwa gramu 10,174.92 zenye thamani ya shilingi 721,750,000. Minada hiyo inaendeshwa na Tume ya Madini kwa kushirikiana na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), kupitia mfumo wa mauzo ya kielektroniki.
Ameongeza kuwa, kutokana na mwenendo wa uzalishaji, mnada wa majaribio wa kimataifa unatarajiwa kufanyika Dubai wiki ya kwanza ya Novemba 2026, huku minada ya ndani ikipangwa kuendelea Desemba 2026, Januari 2027 na Mei 2027.
Ziara hiyo imelenga kujifunza na kutathmini shughuli za uchimbaji, biashara na uongezaji thamani wa madini zinazofanyika ndani ya Ukuta wa Mirerani.
Katika ziara hiyo, Kamati iliambatana na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, pamoja na viongozi na watendaji kutoka Tume ya Madini, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Wilaya ya Simanjiro, Halmashauri na madiwani.
Hatua za kuimarisha tafiti za madini, kuboresha huduma za msingi, kudhibiti utoroshaji na kuongeza fursa za uwekezaji zinatarajiwa kuchangia ukuaji wa shughuli za uchimbaji, kuongeza ajira na kuhakikisha wananchi wananufaika zaidi na rasilimali za madini nchini.



Comments