LUVANDA: MIKOPO YA BENKI INAPASWA KULINDA MAZINGIRA


NA MWANDISHI WETU, MOROGORO 

ASASI ya Kiraia ya SUHODE Foundation ya Morogoro, mshirika wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF), imesema ni muhimu kwa taasisi zote za fedha nchini kuwa na sera madhubuti za kuhakikisha mikopo inayotolewa haiharibu mazingira wala kukiuka haki za binadamu.


Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa SUHODE Foundation, Frank Luvanda, katika mafunzo ya waandishi wa habari juu ya Uendelevu na Uchumi wa Bluu, Uhifadhi na Mazingira.


"Sisi kama asasi za kiraia tumekuwa tukifanya kazi na mabenki na kukutana nao kwa nyakati mbalimbali kupitia WWF. Tunahamasisha mabenki yawe na sera madhubuti ya kuhakikisha kila anayekopa anaeleza dhahiri kuwa hatatumia pesa hizo kuharibu mazingira. Hii ndiyo dhana ya Green Financing," alisema Luvanda.


Luvanda amesema SUHODE Foundation imewezeshwa na WWF kwa muda mrefu kupitia mafunzo, kupelekwa kujifunza kwa vitendo katika maeneo mbalimbali, na wakati mwingine msaada wa kifedha kwa miradi ya uendelevu.


"Sasa tumejikita katika maswala ya uendelevu na ESG - Mazingira, Jamii na Utawala Bora (Environment, Social, Governance) wa sheria zinazosimamia uhifadhi," amesema.


Aidha, Luvanda ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kutoa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kuwawezesha Watanzania asilimia 80 kuachana na nishati chafu.


"Tunapoharibu mazingira tunajiharibia sisi wenyewe. Kesho yetu na ya vizazi vijavyo inakuwa ngumu," amesema.


Alieleza kuwa matumizi ya kuni na mkaa kwa muda mrefu husababisha magonjwa ya njia ya hewa, na wahanga wakubwa ni akina mama wanaopika jikoni.


"Tumekuwa tukihamasisha matumizi bora na sahihi ya nishati. Unaweza kuwa na gesi asilia lakini ukiipikia mahali pa wazi upepo unapuliza, efficiency yake inapungua," alifafanua.


Mkurugenzi huyo amesema SUHODE kwa kushirikiana na WWF na waandishi wa habari wanahamasisha urejeshaji wa maeneo yaliyoharibiwa kwa kupanda miti ya matunda na biashara.


Alitaja mfano wa kupanda miti kando ya mito na milima iliyoharibika, na miti kama miparachichi.


Akizungumzia dhana ya Uchumi wa Kijani na Buluu Luvanda amesema WWF Tanzania wamekuwa machampioni wa dhana hiyo, ambayo ni muhimu kwa jamii.


"WWF imefanya kazi kubwa kuhakikisha bidhaa zote za benki mikopo na nyinginezo zinazingatia uendelevu, ulinzi wa mazingira na bioanuwai. Mikopo inapaswa kuwa na manufaa kwa mkopaji na benki ibaki na sura chanya," amesema.


Kuhusu Uchumi wa Bluu, Luvanda aliipongeza Serikali ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutengeneza sera na miongozo.


"Mfano mzuri ni upumzishaji wa Miamba ya Pweza. Serikali imekubali kutusaidia. Upumzishaji huo umesaidia kuongeza idadi ya Pweza na kipato cha mwananchi. Hata Ziwa Victoria sasa linapumzishwa - samaki anapata kukua na kuzaliana," amesema.


Luvanda alihitimisha kwa kushukuru WWF, asasi za kiraia na Serikali za Mitaa, Halmashauri na Majiji kwa kushirikiana kuhakikisha dhana ya uchumi wa bluu na uhifadhi wa mazingira inatekelezwa kwa uzito.





Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MAELFU WAFURIKA TIKTOK LIVE YA DHARURA YA WAZIRI GWAJIMA KUHUSU CHANGAMOTO ZA WANAUME KWENYE NDOA

MWENGE WA UHURU WAMURIKA MIRADI YA MAENDELEO JIMBO LA KWELA

SERIKALI ITAENDEA KUHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI- LONDO

NMB, UDSM waendeleza ushirikiano wa kukuza vipaji