MAPENDEKEZO YA VIJANA YATAPOKELEWA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA, KUKABILIANA NA MIMBA ZA UTOTONI - PROF. SHEMDOE
NA OWM–TAMISEMI, ARUSHA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema Serikali itapokea na kufanyia kazi mapendekezo ya vijana yanayolenga kuboresha huduma za afya ya msingi katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya, kupitia mfumo wa Serikali wa kupanga mipango kwa kushirikisha wananchi wa Fursa na Vikwazo kwa Maendeleo (O&OD).
Prof. Shemdoe amesisitiza umuhimu wa kusikiliza maoni ya vijana akieleza kuwa asilimia 90 ya vijana hupata huduma za afya katika vituo vya afya ya msingi. Hata hivyo, vijana wenye umri wa miaka 10–24, ambao ni asilimia 31 ya Watanzania milioni 61, bado wanakabiliwa na changamoto za huduma za afya zisizo rafiki kwao, ikiwemo mimba na ndoa za utotoni.
Prof. Shemdoe amesema hayo Oktoba 23, 2026, jijini Arusha, wakati akifungua mjadala unaoongozwa na vijana wa Tanzania kuhusu afya ya uzazi na afya ya akili, ulioandaliwa na Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA).
“Niwatake vijana kutumia siku hizi mbili vizuri na kuja na mapendekezo yanayotekelezeka, yenye muda maalumu wa utekelezaji, ili yapimwe na, pale inapowezekana, yaandaliwe mipango na bajeti kwa ajili ya utekelezaji,” ameeleza Prof. Shemdoe.
Aidha, Prof. Shemdoe amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya afya ya msingi, hivyo amewataka vijana kuilinda ili iendelee kuhudumia wananchi na vizazi vijavyo.
Pia, amewahimiza kupata elimu ya afya ya mama na mtoto ili kumuunga mkono Rais kwa vitendo, akimtaja kuwa kinara wa afya ya mama na mtoto barani Afrika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ECSA, Dkt. Ntuli Kapologwe, amesema vijana wenye umri chini ya miaka 24 katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo ni asilimia 65. Ameeleza kuwa kuwawezesha kupata elimu ya afya ya akili na afya ya uzazi kutasaidia kupunguza vifo vya kina mama na watoto, pamoja na kuhamasisha wanawake kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Naye, Mwakilishi wa Vijana wa Mtandao wa ECSA, Dkt. Kuduishe Kisowile, amesema sehemu kubwa ya vifo vya kina mama inahusishwa na mimba za utotoni na za vijana ambao hawajafikia umri unaofaa. Ameeleza kuwa vijana watashiriki kujadili namna ya kuzuia vifo hivyo na kuimarisha ushirikiano kati ya wizara mbalimbali katika kutokomeza mimba za utotoni.
Mkutano huo umewakutanisha vijana takribani 200 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani kwa lengo la kujadili afya ya uzazi kwa vijana, afya ya akili na utekelezaji wa afua mbalimbali zinazosimamiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, zikiwemo kuhakikisha hakuna mama anayejifungua nyumbani, kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi na kuhakikisha kila mtoto au mtu mzima anayehitaji chanjo anaipata.







Comments