NA MWANDISHI WETU
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa, amezihimiza taasisi za majeshi nchini kusajili na kulinda bunifu zao kisheria ili kutambua umiliki wake, kuzuia matumizi yasiyoidhinishwa na kuongeza thamani ya bidhaa na huduma zinazozalishwa.
Nyaisa ameyasema hayo leo, Oktoba 12, 2026, wakati akifungua mafunzo kuhusu Miliki Ubunifu kwa Majeshi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyofanyika mkoani Morogoro.
Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea maafisa wa majeshi uelewa kuhusu aina mbalimbali za miliki ubunifu zinazoweza kulindwa kisheria, zikiwemo alama za biashara na huduma (nembo), hataza za uvumbuzi, maumbo bunifu, na nyenzo nyingine za miliki ubunifu.
“Kimsingi, mafunzo haya yataangazia umuhimu na mchango wa miliki ubunifu katika taasisi za majeshi nchini, ikiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza. Tutaangalia namna bunifu zinavyoweza kusajiliwa na kulindwa, pamoja na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na huduma zinazotolewa na taasisi hizi zinatambulika na kulindwa kisheria,” amesema Nyaisa.
Ameongeza kuwa uelewa kuhusu miliki ubunifu utasaidia taasisi hizo kutambua na kulinda haki zao juu ya bunifu wanazozalisha, huku ukifungua fursa za matumizi ya bunifu hizo katika kuboresha bidhaa na huduma zao.
Katika hatua nyingine, . Nyaisa ameipongeza Mzinga Corporation kwa hatua ya kusajili na kulinda kisheria ubunifu wa kifaa kinachotumia pilipili kufukuza tembo bila kusababisha madhara kwa binadamu na mazingira, kinachojulikana kama “Pepper Thunder Flash Device.”
“Kipekee, niwapongeze Mzinga Corporation kwa kuchukua hatua ya kulinda ubunifu wao kisheria. Mfano huu unaonesha umuhimu wa taasisi kutambua thamani ya bunifu zinazozalishwa na kuhakikisha zinapata ulinzi unaostahili,” amesema Bw. Nyaisa.
Kwa upande wake, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Magereza Makao Makuu, Bw. Kitila Kitandu, ameishukuru BRELA kwa kuandaa mafunzo hayo, akieleza kuwa taasisi za majeshi hazijihusishi na majukumu ya kiusalama pekee, bali pia uzalishaji wa bidhaa na ubunifu wa teknolojia mbalimbali.
Amesema Jeshi la Magereza linajihusisha na bunifu katika maeneo kama zana za kilimo, ujenzi na utunzaji wa mazingira, hivyo mafunzo hayo yatasaidia kuongeza uelewa kuhusu namna ya kusajili na kulinda bunifu hizo ili zitambulike kisheria.
Naye Thomas Mabula Kawala kutoka Jeshi la Polisi Tanzania amesema taasisi hiyo, pamoja na jukumu lake la kulinda usalama wa raia na mali zao, pia inatekeleza shughuli mbalimbali za uzalishaji na utoaji huduma, ikiwemo ujenzi, huduma za kifedha kupitia vyama vya ushirika vya kuweka na kukopa (SACCOS), pamoja na ushonaji wa sare.
Amesema mafunzo hayo ni fursa ya kujifunza namna ya kusajili na kulinda bunifu zinazotokana na shughuli hizo, sambamba na kupata maarifa mapya yatakayosaidia kuboresha uzalishaji na kuongeza thamani ya bidhaa na huduma zinazotolewa na taasisi hiyo.
Warsha hiyo ya siku mbili inafanyika ikijumuisha majeshi ya Magereza, Polisi, Jeshi la Kujenga taifa, na Jeshi la Wanachi wa Tanzania.




Comments