MRADI WA TOAM, PELUM WAKOSHA MAOFISA KILIMO, WAKULIMA



MAOFISA Kilimo na wakulima kutoka Wilaya za Arusha na Chamwino mkaoni Dodoma wamesema Mradi wa

Kuimarisha Kilimo Ikolojia Hai ili kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, Kupanua Masoko na Usalama wa Chakula Tanzania umekuja wakati muafaka na wataunga  mkono.


Mradi huo wa miaka miwili unatekelezwa katika Halmashauri ya Arusha na Chamwino na Taasisi Kivuli ya Kilimo Hai Tanzania (TOAM) kwa kushirikiana na PELUM Tanzania chini ya ufadhili wa Climate Works na unalenga kuwakutanisha wakulima na wanunuzi ili mazao ya kilimo ikolojia hai yapate soko.


Mtaalamu wa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Bosco Shelle amesema mradi huo umekuja wakati muafaka, kwa sababu utatatua kilio cha muda mrefu cha wakulima kuhusu kukosa soko la uhakika.


Amesema kilio kikubwa cha wakulima wa kilimo ikolojia hai ni namna ya kupata masoko ya uhakika, hivyo wanaona muarubaini umepatikana


"Kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha wakulima wanaodeal na kilimo ikolojia wakiwa wanalia kwenye namna gani wanaweza wakapata masoko ya uhakika. Kwa kupitia mradi huu, wakulima wanaweza wakajengewa uwezo na kupatiwa masoko na kuunganiswa, amesema Shelle.


Amesema kilio hicho hakitaisha moja kwa moja, lakini kitapungua kwa kiasi kikubwa kwani wakulima wakikutana na wanunuzi na kukaa pamoja, watajua watalima wapi na watauza wapi mazao yao.


Shelle alifafanua kuwa Chamwino ina kaya zisizopungua 100,000 na asilimia 95 ya wakulima wanajishughulisha na kilimo. Mazao makuu ni ufuta, alizeti, mahindi, zabibu, uwele, karanga na dengu kwa kiasi kidogo.


"Uzalishaji ni mzuri na unaendelea kuboreka mwaka hadi mwaka. Mradi huu unaenda kuboresha zaidi kwenye upande wa masoko, kwa sababu uzalishaji unafanyika vizuri," amesema.


Mkuu wa Idara ya Kilimo, Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Bahati Mtweve, amesema mradi huo umepokelewa kwa furaha kwa sababu utakamilisha Mradi wa Kilimo Endelevu uliokuwepo Arusha DC.


"Tunaufurahia mradi huu kwa sababu umeingia kwenye kipengele ambacho ni changamoto kubwa kwenye jamii, ambayo ni swala la masoko. Mradi uliopita ulitupa mengi kuhusu kilimo ikolojia, lakini tulikuwa tunatamani wadau wengine waje kujaza pengo la soko," amrsema Mtweve.


Amesema Arusha ina wakulima chini ya 1,000 wa kilimo ikolojia hai kwa sasa, kwa sababu mradi uliopita ulikuwa kwenye vijiji vichache tu.



"Sasa tumepata mwamko. Tumeanza kuhamasisha kwenye vijiji vilivyo nje ya mradi na tumeweka kwenye mipango ya maofisa ugani kutoa elimu ya kilimo ikolojia. Kila ofisa anatakiwa atoe elimu ya kilimo ikolojia," amesema.


Mtweve aliongeza kuwa idadi ya wakulima itaongezeka, lakini kwa kiasi kidogo kwa sababu bado kuna changamoto ya uelewa kwa wakulima wenyewe na kwa walaji.


"Ili wakulima wapate motisha ya kuendelea kuzalisha bidhaa za kikolojia, inategemea sisi walaji tunaitikiaje," amesema.


Mkulima Flora Mollel amesema elimu ya kilimo ikolojia imewameshachemsha na kuwapika vya kutosha na sasa wanachohitaji ni soko la uhakika la mazao yao na kuunganishwa na wanunuzi.


"Tumepikwa tukapikika, tukaiva, mradi huu umekuja wakati sahihi, kwani eneo la masoko ni changamoto kubwa," amesema.


Mkulima huyo amesema wakulima wamefundishwa sana na sasa wanahitaji vitendo. "Sisi kule Arusha tunaona kama uendeshaji wetu uko nyuma. Tumepikwa, tumepikika, tumeiva jamani. Naomba wawezeshaji wetu wafanye namna hii," amesema mkulima huyo.


Kwa upande wake, mkulima Lengo Daudi Ebo kutoka Chamwino amesema mkulima anahitaji kujua soko kabla ya kuingia shambani.


"Kuna mchongo, kuna soko. Ukipata mchongo, ndio utakao nifanya niingie shambani zaidi. Hata wewe ukiwa sehemu yoyote, tusaidiane katika vichwa vyetu kwamba tutaangaliana," amesema Ebo.


Alishukuru waandaaji wa mradi na kusema kama angeanza mapema kilimo ikolojia hai, changamoto nyingi angezishinda.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MAELFU WAFURIKA TIKTOK LIVE YA DHARURA YA WAZIRI GWAJIMA KUHUSU CHANGAMOTO ZA WANAUME KWENYE NDOA

MWENGE WA UHURU WAMURIKA MIRADI YA MAENDELEO JIMBO LA KWELA

NMB, UDSM waendeleza ushirikiano wa kukuza vipaji

SERIKALI ITAENDEA KUHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI- LONDO