NAPE AWASILISHA AZIMIO LA BUNGE LA KUMPONGEZA RAIS SAMIA KUWEZESHA MKUTANO MKUU KUFANYIKA NCHINI

 

MAELEZO KUHUSU AZIMIO LA BUNGE LA KUMPONGEZA MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWA KURIDHIA NA KUWEZESHA KUFANYIKA KWA MKUTANO MKUU WA 153 WA UMOJA WA MABUNGE DUNIANI (IPU) ULIOFANYIKA JIJINI ARUSHA KUANZIA TAREHE 5 – 9 OKTOBA 2026

_____________________________

 

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 64 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge za Mwaka 2025, naomba kuwasilisha Hoja kwamba, Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha Azimio la Bunge la Kumpongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Kuridhia na Kuwezesha kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) uliofanyika Jijini Arusha kuanzia Tarehe 5 – 9 Oktoba 2026.

 

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama leo hii mbele ya Bunge lako Tukufu, na pili kukushukuru wewe binafsi kwa kuruhusu na kunipatia fursa hii adhimu ya kuwasilisha Hoja ya Azimio hili.

 

Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua fursa hii kutoa pongezi za dhati kwa Rais wetu Mpendwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake uliotukuka na wa makini uliowezesha kupatikana kwa mafanikio makubwa ya Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Jijini Arusha. Pamoja na kuwa kwenye maombelezo ya msiba wa mume wake mpendwa (tunamwomba Mwenyezi Mungu ampe pumziko la amani) bado alionesha ustahimilivu na uzalendo mkubwa katika kipindi hiki kigumu kwa kutoa ushirikiano kamili uliowezesha Mkutano huu wa kihistoria kufanyika kwa mafanikio makubwa na kuendelea kuiletea nchi yetu heshima.

 

Mheshimiwa Spika, Tanzania imekuwa mwenyeji wa Mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa IPU mwaka 1889. Mkutano huo wa 153 ulifanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha kuanzia tarehe 5 – 9 Oktoba, 2026. Mkutano huu haukuwa Mkutano wa kawaida wa Kimataifa bali ilikuwa ni tukio la kihistoria kwa Tanzania, hatua muhimu kwa uwakilishi wa Afrika katika uongozi wa Taasisi za Kimataifa, na fursa ya kuthibitisha uimara na nafasi ya Tanzania katika Diplomasia ya Mabunge, Imani ya Tanzania katika Amani, Demokrasia, Utawala Bora na Ushirikiano wa Mataifa. Mkutano huu ulifanyika chini ya Kaulimbiu ya “Kuimarisha Utawala Bora na Kuziwezesha Jamii Kupitia Ushirikishwaji, Uaminifu na Fursa kwa Wote.”

 

Mheshimiwa Spika, Mkutano wa 153 wa IPU ulifunguliwa rasmi tarehe 5 Oktoba, 2026 na Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ufunguzi huo ulihudhuriwa na washiriki wa Mkutano ambao ni Maspika, Wabunge, Watumishi na Wanahabari kutoka duniani kote. Katika ufunguzi huo, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwakaribisha washiriki wote kupitia ujumbe wa video uliorekodiwa mahsusi kwa ajili hiyo.

Mheshimiwa Spika, Mkutano huu ulikuwa ni ushahidi tosha wa imani ya Dunia kwa Tanzania juu ya uumini wake kwa misingi muhimu inayosimamiwa na Umoja wa Mabunge Duniani (Inter-Parliamentary Union-IPU), ambayo misingi yake ni Demokrasia, Amani na Usalama, Haki za Binadamu, Utawala Bora na Diplomasia ya Kibunge.

 

Mheshimiwa Spika, niruhusu sasa niseme kwa kifupi mafanikio yaliyopatikana kwa Taifa kufuatia Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukubali Tanzania kuwa Mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU): -

 

1.           Historia imeandikwa kwa Tanzania kuwa Mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa IPU kwa mara ya kwanza

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali, ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano huu wa IPU tangu kuanzishwa kwake. Hata hivyo, mafanikio ya maandalizi na uendeshaji wa Mkutano huu, yameonesha uwezo mkubwa wa Tanzania wa kuratibu Mikutano mikubwa ya Kimataifa na kuwa jukwaa la majadiliano kuhusu masuala yanayoigusa dunia.

 

2.           Kuonesha Uongozi Bora na Usimamizi Thabiti wa Diplomasia ya Tanzania Duniani chini ya Rais

Mheshimiwa Spika, imani iliyoonyeshwa na Dunia kupitia Taasisi muhimu ya Dunia, Umoja wa Mabunge Duniani na kuipa heshima Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 153 wa IPU, ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi mahiri wa  Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuimarisha misingi ya utawala bora na kuimarika kwa diplomasia ya Tanzania Duniani.

 

3.           Kuimarika kwa nafasi ya Tanzania katika Diplomasia ya Kimataifa

Mheshimiwa Spika, Mkutano wa 153 wa IPU ulihudhuriwa na Washiriki wapato 2044 kutoka zaidi ya nchi 150. Kati ya hao Maspika ni 56, Manaibu Spika 51 na Wabunge 624. Wengine ni Sekretarieti ya IPU, Watumishi wa Mabunge na Waandishi wa Habari. Ushiriki wa Viongozi wa Mabunge mbalimbali duniani, akiwemo Spika wa Bunge la Uingereza, Sir Lindsay Hoyle, umefungua fursa za kuimarisha mahusiano baina ya Bunge la Tanzania na Mabunge ya mataifa mengine. Mkutano huu umeipa Tanzania nafasi ya kuonesha uwezo wake wa kuandaa mikutano ya kimataifa, ukarimu wa wananchi wake, na dhamira yake ya kuendeleza ushirikiano wa kimataifa.

 

1.           Wageni wa Kimataifa Wajionea Hali Halisi ya Nchi na Kuondoa Taswira Hasi

Mheshimiwa Spika, moja ya mafanikio makubwa ya Mkutano huu ni kufanikiwa kubadilisha mtazamo juu ya upotoshaji na kutoa picha halisi ya nchi yetu tofauti na inavyoripotiwa mara kwa mara na vyombo vya habari. Kupitia ushiriki wao wa moja kwa moja, wageni na wajumbe wa kimataifa wameweza kujionea wenyewe amani, usalama, na maendeleo yaliyopo nchini, badala ya kutegemea taarifa za upotoshaji zilizokuwa zikitolewa na upande mmoja. Mkutano huu umewajengea uelewa mpya na wa kweli kuhusu nchi yetu, na kuwa mabalozi wazuri wa kusimulia ukweli halisi kwa jamii za kimataifa wanakotoka. Mfano mzuri ni Spika wa Bunge la Uingereza, ambaye ni mara yake ya kwanza kufika Tanzania; alipongeza sana amani, utulivu na kazi kubwa za maendeleo zinazofanyika nchini, huku akiahidi kurejea tena Tanzania.

 

2.           Kuimarisha Hadhi ya Arusha kama Kitovu cha Diplomasia na Majadiliano ya Kimataifa na Ushirikiano wa Mabunge

Mheshimiwa Spika, Arusha si Jiji la Mikutano pekee, bali ni Jiji lenye historia kubwa katika harakati za ukombozi wa Afrika, 

ushirikiano wa kikanda, haki za binadamu na juhudi za kutafuta suluhu za migogoro kwa njia ya mazungumzo. Arusha ni Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Makao ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu. Hivyo, kwa kuandaa Mkutano Mkuu wa 153 wa IPU, Tanzania imeongeza fursa za kuitangaza Arusha kama Kitovu cha Diplomasia, Majadiliano ya Kimataifa na Ushirikiano wa Mabunge.

 

1.           Mchango katika Amani, Usalama na Demokrasia Duniani

Mheshimiwa Sipka, katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na migogoro ya kivita, migawanyiko ya kisiasa, changamoto za Mabadiliko ya Tabianchi na kupungua kwa imani ya wananchi kwa baadhi ya Taasisi za Umma, Mkutano wa Arusha umetoa Jukwaa la Majadiliano na kutafuta misingi ya makubaliano. Mkutano huu umesisitiza umuhimu wa diplomasia ya kibunge, utatuzi wa migogoro kwa njia za amani, kuheshimu sheria za kimataifa, na kuimarisha taasisi za kidemokrasia. Hivyo, Majadiliano kuhusu haki za binadamu, watu wenye ulemavu, mabadiliko ya tabianchi na teknolojia zinazoibukia yameonesha wajibu wa Mabunge katika kutafuta majibu ya changamoto zinazowakabili wananchi.

 

2.           Kuimarika kwa Ushiriki wa Wanawake katika Mabunge Duniani

Mheshimiwa Spika, Mkutano wa Arusha umeweka rekodi ya ushiriki wa wanawake, ambao walifikia asilimia 39.4 ya Wabunge waliohudhuria Mkutano huo. Hatua hii, ikiunganishwa na historia ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, inatukumbusha umuhimu wa kuendelea kuongeza nafasi za Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu katika uongozi na maamuzi.1.           Umuhimu wa Tamko la Arusha (Arusha Communique)

Mheshimiwa Spika, Mkutano huu umeacha urithi muhimu kupitia Tamko la Arusha, linalosisitiza utawala bora, ushirikishwaji, uaminifu na fursa kwa wote. Tamko hili linatukumbusha kwamba thamani ya demokrasia haipimwi kwa uwepo wa taasisi pekee, bali pia kwa namna taasisi hizo zinavyoboresha maisha ya wananchi. Kwa hiyo, mafanikio ya Mkutano huu hayapaswi kuishia kwa kutoa pongezi pekee, bali yanapaswa kuendelezwa kupitia sheria bora, uwajibikaji, usimamizi wa Serikali na ushirikishwaji wa wananchi.

 

2.           Kuchangia katika uchumi wa Taifa hususan Jiji la Arusha katika eneo la hoteli, usafiri wa anga, biashara na ajira

Mheshimiwa Spika, kutokana na uwepo wa Mkutano wa 153 wa IPU hoteli za Arusha zilipata fursa ya kuhudumia Wajumbe na wageni wengi wa Mkutano na hivyo kuongeza mzunguko wa fedha na ajira katika sekta hiyo; kuongezeka kwa mahitaji ya safari za ndege kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na Uwanja wa Ndege wa Arusha ilitoa fursa kwa watoa huduma za usafiri kupata mapato kutokana na safari za wageni na shughuli za Mkutano pamoja na wafanyabiashara wadogo na wa kati, wakiwemo wauzaji wa chakula, wajasiriamali wa bidhaa za utalii kupata fursa ya kuwafikia wateja wa Kimataifa.

 

Mheshimiwa Spika, historia haiyakumbuki Mataifa kwa idadi ya Mikutano iliyofanyika katika ardhi yake pekee bali inayakumbuka kwa mawazo yaliyotolewa, madaraja ya ushirikiano yaliyojengwa, na mchango wake katika maendeleo ya binadamu. Katika Mkutano wa 153 wa IPU, Tanzania haikuwa mwenyeji wa wageni pekee; bali ilikuwa mwenyeji wa majadiliano kuhusu mustakabali wa dunia, huku Watanzania wawili wakiandika historia katika uongozi wa taasisi hii ya Kimataifa. Hivyo, tumeikaribisha dunia  Arusha; sasa jukumu letu ni kuhakikisha maamuzi yaliyofanyika Arusha yanachangia kuijenga dunia bora zaidi.

 

Mheshimiwa Spika, nimalizie maelezo yangu ya utangulizi kwa kutambua mchango wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Azzan Zungu, Katibu wa Bunge, Ndg. Baraka I. Leonard na Kamati nzima ya Maandalizi kwa kazi kubwa katika kuongoza na kuratibu maandalizi yaliyowezesha kufanikisha Mkutano huu.

 

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, kwa mujibu wa Kanuni ya 64 (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, naomba sasa niwasilishe Azimio lenyewe kama ifuatavyo:-

 

AZIMIO LA BUNGE LA KUMPONGEZA MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWA KURIDHIA NA KUWEZESHA KUFANYIKA KWA MKUTANO MKUU WA 153 WA UMOJA WA MABUNGE DUNIANI (IPU) ULIOFANYIKA JIJINI ARUSHA KUANZIA TAREHE 5 – 9 OKTOBA 2026

 

KWA KUWA, Tanzania imeandika historia chini ya Uongozi madhubuti wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa IPU kwa mara ya kwanza ambapo mafanikio ya maandalizi na uendeshaji wake yameonesha uwezo wa Tanzania wa kuendesha Mikutano mikubwa ya Kimataifa na kuwa Jukwaa la Majadiliano kuhusu masuala yanayoigusa dunia;

 

NA KWA KUWA, imani iliyoonyeshwa na Taasisi muhimu ya Dunia, Umoja wa Mabunge Duniani kuamua kuipa heshima Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 153 wa IPU ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi Mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuimarisha misingi ya utawala bora na kuimarika kwa diplomasia ya Tanzania Duniani;

 

NA KWA KUWA, ushiriki wa Viongozi wa Mabunge mbalimbali Duniani, wakiwemo Maspika 56 wa Mabunge, umefungua fursa za kuimarisha mahusiano baina ya Bunge la Tanzania na Mabunge ya Mataifa mengine;

 

NA KWA KUWA, Mkutano Mkuu wa 153 umekuwa na Maazimio mbalimbali ikiwemo: Kuimarisha Utawala Bora na kuwezesha jamii kupitia ujumuishi, uaminifu na fursa kwa wote; Maendeleo ya kijamii jumuishi kwa wote: Mikakati ya kibunge ya kukuza haki na uwezeshaji wa Watu wenye Ulemavu; hatua za haraka za kibunge kukabiliana na majanga yanayohusiana na tabianchi na kuimarisha ustahimilivu katika eneo la Himalaya na maeneo mengine yaliyo katika hatari ya majanga; kukuza mustakabali wa kazi unaozingatia haki, ujumuishi na uendelevu katika kipindi cha maendeleo ya Akili Unde (AI); na Umoja wa Mataifa unaokidhi mahitaji ya wakati huu: Kuelekea Mkutano wa mapitio ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa; Masuala ambayo yamekuwa kipaumbele cha Mheshimiwa Rais katika Uongozi wake.

 

KWA HIYO BASI, Bunge hili katika Mkutano wake wa Tano, Kikao cha Kwanza, tarehe 27 Oktoba, 2026 linaazimia kwa dhati na kauli moja :-

 

KWANZA: Kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 153 wa IPU kwa mara ya kwanza na kuwezesha maandalizi na uendeshaji wake.

 

PILI: Kuendelea kuunga mkono dhamira ya Mhe. Rais ya kuimarisha diplomasia ya kibunge, ushirikiano wa Afrika, amani na usalama wa kimataifa, demokrasia, usawa wa kijinsia na maendeleo jumuishi.TATU: Kuhimiza juhudi endelevu za Mheshimiwa Rais katika kuitangaza na kuiendeleza Arusha kama Kitovu cha Mikutano mikubwa, Utalii, Diplomasia na Ushirikiano wa Kimataifa.

 

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja

 

Mhe. Nape Moses Nnauye, Mb.

MBUNGE WA JIMBO LA MTAMA

27 Oktoba, 2026

 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MAELFU WAFURIKA TIKTOK LIVE YA DHARURA YA WAZIRI GWAJIMA KUHUSU CHANGAMOTO ZA WANAUME KWENYE NDOA

MWENGE WA UHURU WAMURIKA MIRADI YA MAENDELEO JIMBO LA KWELA

SERIKALI ITAENDEA KUHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI- LONDO

NMB, UDSM waendeleza ushirikiano wa kukuza vipaji