NMB YATENGA SH. BIL.2 KWA KAMPUNI CHANGA, MAKAMU WA RAIS ATAKA MATOKEO

 Benki ya NMB imetenga Sh bilioni 2 kusaidia kampuni changa za teknolojia, huku ikilenga kuunganisha kampuni 30 na mifumo yake ya kibenki ifikapo mwaka 2030, kutoka sita zilizopo sasa. Benki hiyo pia inatarajia kuanzisha Kituo cha Ubunifu (NMB Innovation Hub) ili kuchochea ukuaji wa biashara bunifu nchini.

Akizungumza katika Tanzania Startup Week 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, amesema kampuni sita tayari zimeanza kuuza suluhisho zao kupitia mifumo ya benki hiyo, huku nyingine tano zikitarajiwa kuunganishwa kabla ya mwisho wa mwaka. Amesema hatua hiyo inazipa kampuni changa fursa ya kufikia wateja zaidi ya milioni 10 wa NMB.

Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, ameipongeza NMB kwa kuunga mkono ubunifu wa vijana, lakini amesisitiza umuhimu wa kupima matokeo ya uwekezaji huo. Ametaka kuwekwa wazi fedha zilizotumika, idadi ya kampuni zilizonufaika na zilizokua hadi kujiendesha, huku akizitaka taasisi za fedha kusaidia biashara changa zinazokabiliwa na changamoto ya ukosefu wa dhamana za mikopo.

Awali, Meneja wa Ubunifu wa Benki ya NMB, Maria Mwamnyalla, amesema zaidi ya bunifu 300 zimefanyiwa majaribio kupitia NMB Sandbox tangu mwaka 2021. Amesema fedha zilizotengwa zitasaidia kuondoa vikwazo vya kiteknolojia vinavyokwamisha kampuni changa kufikia masoko. NMB imekuwa mdhamini mkuu wa Tanzania Startup Week tangu mwaka 2024.


 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MAELFU WAFURIKA TIKTOK LIVE YA DHARURA YA WAZIRI GWAJIMA KUHUSU CHANGAMOTO ZA WANAUME KWENYE NDOA

MWENGE WA UHURU WAMURIKA MIRADI YA MAENDELEO JIMBO LA KWELA

NMB, UDSM waendeleza ushirikiano wa kukuza vipaji

SERIKALI ITAENDEA KUHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI- LONDO