TAEC, IAEA ZAKUTANISHA WATAALAMU WA NCHI 16 KUDHIBITI MBUNG’O AFRIKA

Na Mwandishi wetu – Arusha

Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), kwa kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu (IAEA), imewakutanisha wataalamu kutoka nchi 16 za Afrika jijini Arusha katika mafunzo ya kikanda yanayolenga kuimarisha utafiti na udhibiti wa mbung’o wanaoeneza magonjwa kwa binadamu na mifugo.

Akifungua mafunzo hayo yanayofanyika katika Hoteli ya Best Western Parrot kuanzia Oktoba 19 hadi 30, 2026, Mkurugenzi wa TAEC, Prof. Najat Mohamed, amesema lengo ni kuwajengea wataalamu uwezo wa kukusanya na kuchambua takwimu za kisayansi zitakazosaidia kubaini maeneo yaliyoathirika na kupanga mikakati madhubuti ya kudhibiti mbung’o.

Amesema mafunzo hayo yanahusu taratibu za ukusanyaji wa takwimu za awali za entomolojia (entomological baseline data collection procedures), ambazo ni muhimu katika utekelezaji wa mipango jumuishi ya kudhibiti wadudu hao katika maeneo mbalimbali ya Afrika.

Prof. Najat amesema washiriki wanapata fursa ya kubadilishana uzoefu wa nchi zao kuhusu changamoto za mbung’o, mbinu zilizotumika kukabiliana nao na matumizi ya takwimu sahihi katika kupanga hatua za udhibiti, ikiwemo kutumia teknolojia za kisasa kama teknolojia ya nyuklia.

Ameeleza kuwa mbung’o ni changamoto inayogusa sekta mbalimbali, ikiwemo mifugo na afya ya binadamu, kwa kuwa wadudu hao wanaweza kueneza ugonjwa wa ndorobo kwa mifugo na kusababisha ugonjwa wa malale kwa binadamu, hali inayoweza kuathiri uzalishaji, kipato na ustawi wa jamii.

“Mbung’o ni miongoni mwa changamoto zinazoathiri uzalishaji wa mifugo na ustawi wa jamii. Hivyo, ni muhimu kutumia takwimu na utafiti wa kisayansi katika kupanga mikakati ya kukabiliana na changamoto hii,” amesema Prof. Najat.

Kwa upande wake, mtaalamu kutoka Kenya, Agnes Ochwani, ambaye ni Mratibu wa Kikanda katika Baraza la Kutokomeza Ugonjwa wa Ndorobo nchini Kenya (CCE Anti-Panosomiasis Eradication Council), amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kushirikiana katika kudhibiti mbung’o. Amesema changamoto hiyo inahitaji mikakati ya pamoja kwa kuwa wadudu hao hawaishii katika mipaka ya nchi moja.

Ochwani amesema ushirikiano kati ya wataalamu na taasisi za nchi mbalimbali ni muhimu katika kubadilishana taarifa, uzoefu na mbinu za udhibiti, akieleza kuwa juhudi za nchi moja haziwezi kufikia matokeo yanayotarajiwa ikiwa nchi nyingine zilizoathirika hazitatekeleza mikakati inayolingana.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuimarisha matumizi ya takwimu za kisayansi katika kufanya maamuzi na kusaidia nchi za Afrika kuweka mikakati endelevu ya kudhibiti mbung’o na kupunguza athari zao kwa binadamu na mifugo.
 
  Kutoka kulia ni Mkurugenzi wa TAEC, Prof. Najat Mohamed, kushoto kwake ni muwakilishi wa IAEA

 
Washiriki wa mafunzo kutoka nchi 16 Barani Afrika

 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MAELFU WAFURIKA TIKTOK LIVE YA DHARURA YA WAZIRI GWAJIMA KUHUSU CHANGAMOTO ZA WANAUME KWENYE NDOA

MWENGE WA UHURU WAMURIKA MIRADI YA MAENDELEO JIMBO LA KWELA

NMB, UDSM waendeleza ushirikiano wa kukuza vipaji

SERIKALI ITAENDEA KUHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI- LONDO