NA MWANDISHI WETU
TAASISI Kivuli ya Kilimo Hai Tanzania (TOAM) na PELUM Tanzania zinatekeleza Mradi wa Kuimarisha Kiliko Ikolojia Hai kwa ajili ya Kukabuliliana na Mabadiliko ya Tabianchi, Kupanua Masoko na Kuhakikisha Usalama wa Chakula.
Hayo yamesemwa na Meneja Miradi wa TOAM, Sandra Haule, wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofanyika mkoani Dodoma Leo.
Amesema mradi huo ni wa majaribio na ni mara ya kwanza kwa TOAM kufanya kazi na mfadhili huyo mpya.
Amesema mradi huo wa miaka miwili wenye thamani ya Dola za Kimarekani 200,000, unaolenga kusaidia wakulima wa kilimo ikolojia hai kupata soko la uhakika la mazao yao, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha usalama wa chakula nchini.
> "Huu ni mradi wetu mpya. Tumepata ufadhili wa mdau mpya wa maendeleo anayeitwa Climate Works kutoka Marekani. Ni mradi wa miaka miwili na wenye thamani ya Dola 200,000," amesema Haule.
Haule amesema mradi huo unatekelezwa katika Halmashauri za Arusha na Chamwino ambazo zimeangukia katika maeneo ya vipaumbele yaliyoainishwa kwenye Mkakati wa Taifa wa Kilimo Ikolojia Hai uliozinduliwa mwaka 2025.
> "Mkakati wa Taifa ulikuwa na malengo 12, lakini wadau walikaa na kuweka vipaumbele sita na kuainisha maeneo matatu ya majaribio: Arusha, Kanda ya Kati ambayo Dodoma inaangukia, na Kanda ya Ziwa ambayo Mwanza inaangukia," amesema.
Aliongeza kuwa kwa vile mradi ni mdogo, walichagua wilaya ambazo tayari zina chachu ya utambuzi wa kilimo ikolojia hai.
> "Tulichagua Wilaya ya Chamwino kwa sababu tumekuwa na mahusiano nayo kwa muda mrefu, zaidi ya miaka 10. Kwa upande wa Arusha, tuna mdau wetu IDP ambaye ni kinara wa kupeperusha bendera ya kilimo hai kanda ya kaskazini. Tukasema tufanye kazi na vikundi vya IDP," amesema.
*Mradi Utaanzia Baada ya Uzalishaji*
Haule amesema mradi huu ni tofauti na miradi mingine kwa sababu hauendi kumfundisha mkulima mbinu za kilimo ikolojia hai.
> "Mradi huu unaenda kumsaidia mkulima kuanzia pale ameshamaaliza uzalishaji. Tunafanya kazi na vikundi ambavyo tayari vinafahamu kilimo ikolojia hai ni nini. Tunaenda kuanzia pale kwenye production point," amesema.
Amesema mradi utaangalia changamoto zinazomkabili mkulima katika kupata masoko, na kuangalia upanuzi wa masoko (market access) pamoja na kuunganisha mifumo ya masoko.
> "Kwa hiyo mradi huu unalenga kuangalia upanuzi wa masoko ili mkulima aweze kuuza mazao yake kwa uhakika," amesisitiza.
Mradi huo unatarajiwa kuwa daraja kati ya mkulima na mnunuzi, huku ukihakikisha mazao ya kilimo ikolojia hai yanatambulika na kupata bei nzuri.



Comments