Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Jackson Kiswaga, ameitaka Serikali kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya maji kwa kuhakikisha eneo la hifadhi la mita 60 kila upande linazingatiwa ili kuzuia uharibifu wa mazingira na kulinda rasilimali hizo muhimu.
Kiswaga, ambaye pia ni Mbunge wa Kalenga, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha vyanzo vya maji vinaendelea kutumika kwa shughuli mbalimbali, ikiwemo uzalishaji wa nishati ya umeme kupitia mabwawa.
Aidha, amesema kamati hiyo imeishauri Wizara ya Maji kushirikisha sekta binafsi katika ujenzi wa miradi mipya, hususan katika miji mikubwa inayokabiliwa na upungufu wa huduma hiyo.
Amesema upatikanaji wa maji katika maeneo husika umefikia asilimia 66, huku asilimia 34 ya mahitaji ikiwa bado haijafikiwa.
Miji aliyoitaja kukabiliwa na changamoto hiyo ni Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Morogoro na Arusha.
Kiswaga ameyasema hayo katika viunga vya Bunge jijini Dodoma, Oktoba 20, 2026, baada ya kumalizika kwa vikao vya kamati hiyo na Wizara ya Maji.

Comments