WANAFUNZI 50,000 WANUFAIKA NA PROGRAMU YA UWEKEZAJI YA DSE


NA MWANDISHI WETU

Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limewafikia jumla ya washiriki 50,000 tangu kuanzishwa kwa programu ya DSE Scholar Investment Challenge mwaka 2014, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha elimu ya fedha na uwekezaji kwa vijana nchini.


Katika msimu wa 2025/2026, programu hiyo imewashirikisha wanafunzi 7,883 kutoka taasisi mbalimbali za elimu, huku wanafunzi 10 wakifanikiwa kufika hatua ya fainali.


Akizungumza katika fainali ya DSE Scholar Investment Challenge 2025/2026 iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam amesema programu hiyo inalenga kuwajengea vijana uelewa wa masoko ya mitaji, uwekezaji, akiba na maamuzi sahihi ya kifedha.


Amesema idadi hiyo ya washiriki inaonesha umuhimu wa kuendeleza utamaduni wa uwekezaji miongoni mwa vijana, ambao ni sehemu muhimu ya kujenga uchumi imara na wenye ushindani.


Ameeleza kuwa soko la mitaji halipaswi kuonekana kuwa eneo la wataalamu pekee, bali ni sehemu ya uchumi inayoweza kuwapa wananchi fursa za uwekezaji na kusaidia kampuni kupata mitaji ya kukuza biashara, kuanzisha miradi na kutengeneza ajira.


Aidha, DSE imeendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia kupitia mfumo wa Hisa Kiganjani, unaolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za biashara ya hisa na kupanua wigo wa wawekezaji wanaoweza kushiriki katika soko hilo.


Kwa mujibu wa hotuba hiyo, thamani ya miamala ya hisa katika DSE ilifikia Shilingi bilioni 824.08 katika robo ya tatu ya mwaka 2026, ikiwa ni ongezeko la asilimia 231.2 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 248.64 zilizorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2025.


Vilevile, mtaji wa soko ulifikia Shilingi trilioni 40.57 kufikia Septemba 30, 2026.


Amesema takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika mifumo ya kidijitali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za soko la mitaji, huku akisisitiza kuwa elimu ya uwekezaji ni muhimu ili kuwasaidia wananchi kuelewa fursa na hatari zinazohusiana na uwekezaji.


Ameongeza kuwa lengo la DSE si kuwahamasisha vijana kuwekeza bila maandalizi, bali kuwapatia maarifa yatakayowawezesha kuelewa hatari na kufanya maamuzi yanayozingatia uwezo na malengo yao ya kifedha.



Akizungumzia mchango wa programu hiyo katika maendeleo ya taifa, alisema DSE Scholar Investment Challenge inaunga mkono matarajio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ya kujenga uchumi wenye ushindani, unaochochea ubunifu na kupanua fursa za kiuchumi kwa wananchi.


Amesema pia programu hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa DSE wa mwaka 2023–2027, unaolenga kupanua upatikanaji wa huduma za soko la mitaji, kuimarisha mifumo ya kidijitali na kuongeza ushiriki wa wawekezaji.


Amebainisha kuwa kupitia programu hiyo, wanafunzi wanapata nafasi ya kujifunza kwa vitendo namna masoko ya mitaji yanavyofanya kazi, jinsi ya kutumia taarifa katika kufanya maamuzi na uhusiano uliopo kati ya faida na hatari katika uwekezaji.


Aidha, amewataka wanafunzi walioshiriki katika mashindano hayo kuendeleza maarifa waliyopata kwa kuwahamasisha wenzao, familia na jamii kuhusu umuhimu wa kuweka akiba, kuwekeza na kutumia fedha kwa uangalifu.


Katika hatua nyingine, DSE imesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za elimu, benki, madalali wa soko la hisa, kampuni na wadau wa maendeleo ili kupanua wigo wa elimu ya fedha na uwekezaji nchini.


Afisa huyo aliwashukuru wadhamini, washirika, walimu, wazazi na taasisi za elimu kwa mchango wao katika kufanikisha programu hiyo na kuwapa wanafunzi fursa ya kupata maarifa kuhusu masoko ya mitaji.


Pia aliwapongeza wanafunzi wote 7,883 walioshiriki katika msimu wa mwaka 2025/2026, huku akiwatakia mafanikio wanafunzi 10 waliofika hatua ya fainali.


Alisisitiza kuwa mafanikio makubwa ya programu hiyo hayapaswi kupimwa kwa washindi pekee, bali pia kwa maarifa ambayo wanafunzi wanayapata na namna wanavyoweza kuyatumia katika maisha yao ya sasa na ya baadaye.


Alisema DSE itaendelea kuimarisha elimu ya fedha, kuboresha huduma za kidijitali na kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuwafikia wawekezaji wapya na kuwawezesha kushiriki katika soko la mitaji wakiwa na uelewa wa kutosha.


Alimalizia kwa kusisitiza kuwa vijana wanapaswa kuwa sehemu ya ujenzi wa uchumi wa kesho kwa kuanza kujifunza na kutumia maarifa ya kifedha tangu sasa.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MAELFU WAFURIKA TIKTOK LIVE YA DHARURA YA WAZIRI GWAJIMA KUHUSU CHANGAMOTO ZA WANAUME KWENYE NDOA

MWENGE WA UHURU WAMURIKA MIRADI YA MAENDELEO JIMBO LA KWELA

SERIKALI ITAENDEA KUHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI- LONDO

NMB, UDSM waendeleza ushirikiano wa kukuza vipaji