![]() |
NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
SHIRIKA la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF), Kupitia Program ya Marine inayotekeleza shughuli za usimamizi maeneo ya Bahari na Pwani imewezesha zaidi ya wanavijiji 15,300 katika Wilaya za Kibiti, Mafia, Rufiji mkoani Pwani na Kilwa mkoani Lindi kujikwamua kiuchumi kupitia Vikundi vya Kuweka na Kukopa (VICOBA) na kutunza mazingira.
Wanavijiji hao ni wale ambao wapo katika eneo la Hifadhi Hai ya Binadamu na Mazingira inayoitwa RUMAK inayohusu Wilaya nne za Mafia, Rufiji, Kilwa na Kibiti, lenye hekta takribani milioni 1.
Hayo yamebainishwa na Ofisa Mikopo na Biashara wa WWF, James Golola, wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii katika warsha ya siku tatu, iliyofanyika mkoani Morogoro kwa kuandaliwa na shirikika hilo.
Amesema lengo kubwa la RUMAK ni kukuza uchumi, utamaduni na ikolojia.
"Hifadhi Hai maana yake ndani yake lazima wawemo binadamu wanaendelea na shughuli zao kama kawaida. Pamoja na kuhifadhi mazingira, binadamu wanazitumia rasilimali kwa njia endelevu. Ndani yake kuna utalii, uvuvi, kilimo cha mwani, ufugaji wa nyuki na majongoo bahari," amesema.
Golola amesema WWF wamefanikiwa kugusa kundi kubwa la wananchi kwa kutengeneza sera, miongozo ya kufunga na kufungua miamba Pweza, isimamizi wa mikoko na na mipango wa usimamizi wa uvunaji wa mwani.
"Kazi yetu kuu ni uhifadhi, lakini anayehifadhi ni binadamu. Huwezi kumwambia mtu ahifadhi wakati hana chakula," amesema Golola.
Amesema WWF kuanzia 2006 hadi sasa imeanzisha vikundi 605 vya Community Microfinance Groups (CMG) na Vikoba vyenye wanachama 15,300 ambavyo kwa sasa vina mtaji wa Sh Bilioni 17 na vimetoa
mikopo ya zaidi ya Sh Bilioni 18.
"Mtu sasa anakula milo mitatu, amejenga nyumba za kisasa, wengine mpaka lodge. Tulianza kwa kuwapa elimu, sio pesa. Methali inasema - usimpe samaki, mfundishe kuvua," amesema Golola.
Ofisa huyo amesema mbali na vikoba, WWF inasaidia vikundi vya ujasiriamali ufugaji nyuki, kilimo cha mwani, ufugaji majongoo bahari, na unenepeshaji kaa. Inawapa boti, mashine za kusaga mwani, na mafunzo ya kutengeneza sabuni, mafuta na unga wa mwani.
Pia amesema WWF imeanzisha Vikundi vya Usimamizi wa Rasilimali za Pwani na Bahari (BMU) 72 na Kamati ya Usimamizi Eneo la Pamoja la Uvuvi (CFMA), ambazo zimekuwa na tija kubwa.
"BMU inaundwa na wadau wote wanaotumia rasilimali za uvuvi, wavuvi, wachakataji, mama lishe. Ina kamati za Takwimu, Doria, na Mipango na Fedha. Kazi yake ni kuhakikisha sheria za uvuvi zinafuatwa," amesema Golola.
Amesema tangu 2006 hadi sasa, WWF imefanya kazi katika wilaya sita - Mtwara Vijijini, Kilwa, Kibiti, Mafia, Mkuranga na Rufiji, pamoja na Pemba.
Ofisa huyo amesema jamii ikihifadhi matumbawe na nyasi bahari, mazalia ya samaki yanaongezeka, dagaa na samaki, Papa Potwe wanaongezeka.



Comments