DCEA YANASA VINARA WANAODAIWA KUHUSIKA DAWA ZA KULEVYA


 NA MWANDISHI WETU


MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na mamlaka za usalama nchini Kenya, imefanikiwa kuvunja mitandao ya kimataifa ya biashara na usafirishaji wa dawa za kulevya, kufuatia operesheni zilizofanyika Tanzania na Kenya na kukamata jumla ya paketi 753 za dawa hizo.

Kamishna wa Mamlaka hiyo, Aretas Lyimo, amebainisha hayo leo Novemba 9, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungunza na Waandishi wa Vyombo mbalbali vya Habari.

Aidha amesema anashangwaza dawa hizo mikapani licha ya kuwepo utaratibu wa ukaguzi hali inayoaminika wapo baadhi ya watendaji hujipofusha macho na kusisitiza mipango madhubuti inawekwa ili kudhibiti uingiaji wake kupitia mipakani.


Amesema operesheni ya kwanza iliyofanyika Novemba 6, 2026, eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam, DCEA ilikamata jumla ya paketi 299 za dawa za kulevya, zikiwemo paketi 24 za heroin na paketi 275 za methamphetamine. Dawa hizo zilikuwa zimefichwa ndani ya magunia ya mahindi na gari aina ya Ford Ranger lenye namba za usajili T.950 ERA na T.417 EJZ.


Kutokana na operesheni hiyo, watuhumiwa wanne walikamatwa ambao ni Juma Slaati Kisomeko (36), raia wa Uganda, dereva na mkazi wa Pii nchini Uganda; Issa Said Nassor (34), mfanyabiashara; Ibrahim Said Chembela (30), dereva; na Mohamed Ally Shemtuu (45), dereva. Watuhumiwa watatu wa mwisho ni wakazi wa Tabata jijini Dar es Salaam.


Baada ya kukamatwa na kuhojiwa, watuhumiwa hao walieleza kuwa dawa hizo walizichukua Mombasa nchini Kenya na kuzisafirisha kupitia mpaka wa Horohoro mkoani Tanga. Taarifa hizo ziliwezesha DCEA kuwasiliana na mamlaka za usalama nchini Kenya na kushirikiana katika kubaini chanzo cha dawa hizo pamoja na kuwakamata washukiwa wengine wanaohusika na mtandao huo.


Kupitia ushirikiano huo, Novemba 7, 2026, DCEA kwa kushirikiana na Kitengo cha Kitaifa cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini Kenya (NANB), ilifanya operesheni eneo la Kwale, Mombasa nchini Kenya, ambapo ilikamata paketi 454 za dawa za kulevya aina ya methamphetamine zilizohusishwa na operesheni iliyofanyika Tanzania.


Katika operesheni hiyo nchini Kenya, watuhumiwa wengine watatu walikamatwa ambao ni Saleh Khamis Baseleman (45), maarufu kwa jina la Mbwiga, mfanyabiashara na mkazi wa Mombasa; Seif Said Hamad (54), maarufu kwa jina la Babu Seif, raia wa Tanzania na mfanyabiashara; pamoja na Zuraicah Ahmed Hussein (25), raia wa Uganda, mfanyabiashara na mkazi wa Shirazi, Mombasa nchini Kenya.


Taarifa za uchunguzi zinaonesha kuwa watuhumiwa hao wanadaiwa kuwa sehemu ya mtandao wa kimataifa unaojihusisha na ununuzi na usafirishaji wa dawa za kulevya kutoka Afghanistan kupitia njia za baharini hadi Mombasa nchini Kenya na kisha kuziingiza katika nchi mbalimbali, ikiwemo Tanzania. Mmoja wa watuhumiwa, Saleh Khamis Baseleman, maarufu Mbwiga, anadaiwa kununua dawa hizo nchini Afghanistan na kuzisafirisha kwa njia ya bahari hadi Mombasa. Aidha, anahusishwa na kukamatwa kwa tani 3.5 za dawa za kulevya zilizokamatwa na DCEA Desemba 2023, Kigamboni jijini Dar es Salaam na mkoani Iringa.


DCEA imesema uchunguzi wa kesi hiyo unaendelea kwa kushirikiana na mamlaka za Tanzania na Kenya ili kuhakikisha watuhumiwa wote wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria. Aidha, imeeleza kuwa watuhumiwa hao ni sehemu ya mtandao unaofanya shughuli zake katika nchi mbalimbali, zikiwemo Afghanistan, Afrika Kusini, Msumbiji, Zambia, Malawi, Uganda, Kenya, Tanzania na Dubai, huku ikisisitiza kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu vihatarishi vya uwepo wa biashara na matumizi ya dawa za kulevya.








Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MWENGE WA UHURU WAMURIKA MIRADI YA MAENDELEO JIMBO LA KWELA

MAELFU WAFURIKA TIKTOK LIVE YA DHARURA YA WAZIRI GWAJIMA KUHUSU CHANGAMOTO ZA WANAUME KWENYE NDOA

SERIKALI ITAENDEA KUHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI- LONDO

NMB, UDSM waendeleza ushirikiano wa kukuza vipaji