KAKA WA MWENYEKITI CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) TUNDU LISSU AFARIKI DUNIA

 Dar es Salaam . Alute Mughwai Lissu, kaka wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Selian, mkoani Arusha.


Alute, ambaye alikuwa wakili mwandamizi na kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), amefariki dunia leo Jumapili, Novemba mosi, 2026, baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Mwananchi imezungumza na Rose Masesa, dada wa Lissu, ambaye amethibitisha kifo hicho na kusema Alute alifariki baada ya hali yake kuwa mbaya.

"Ni kweli amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha ya Selian, baada ya kuzidiwa ghafla juzi,” amesema Rose.

Rose, ambaye saa 4 asubuhi alikuwa safarini kutoka Songea, mkoani Ruvuma, kuelekea Arusha, amesema Alute alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa figo kwa kipindi kirefu.


Alikuwa anafanyiwa dialysis. Hata ukimwona akija mahakamani kufuatilia kesi ya Lissu, alikuwa na kitu shingoni. Afya yake haikuwa nzuri sana,” amesema.

Amesema taarifa kuhusu maandalizi ya mazishi zitatolewa baada ya familia kufanya kikao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia, amesema viongozi wa chama hicho walikuwa wakielekea gerezani kuzungumza na Mwenyekiti wao, Lissu, kabla ya kutoa taarifa rasmi kwa umma.


"Taarifa ni za kweli na sasa viongozi wetu wanaelekea gerezani kuonana na Mwenyekiti. Wakirudi, tutatoa taarifa kwa umma,” amesema.

Tundu Lissu anashikiliwa katika Gereza la Ukonga, Dar es Salaam, akikabiliwa na kesi ya uhaini ambayo imekuwa ikiendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja.


Hukumu ya kesi hiyo inatarajiwa kutolewa Ijumaa, Novemba 6, 2026, katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MAELFU WAFURIKA TIKTOK LIVE YA DHARURA YA WAZIRI GWAJIMA KUHUSU CHANGAMOTO ZA WANAUME KWENYE NDOA

MWENGE WA UHURU WAMURIKA MIRADI YA MAENDELEO JIMBO LA KWELA

SERIKALI ITAENDEA KUHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI- LONDO

NMB, UDSM waendeleza ushirikiano wa kukuza vipaji