SPIKA ZUNGU ATUMA UJUMBE KWA NCHI MAZIWA MAKUU

  Na Mwandishi wetu



SPIKA wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, ametuma ujumbe kwa nchi wanachama wa Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) akizitaka kutekeleza kwa vitendo makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa Wabunge wanawake kuhusu amani, usalama na maendeleo.


Akizungumza leo alipokuwa akifunga mkutano wa wanawake wabunge wa Jukwaa la Mabunge la ICGLR uliofanyika Dar es Salaam Spika Zungu amesema mafanikio ya mkutano huo yatapimwa kwa hatua zitakazochukuliwa na nchi wanachama kutekeleza maazimio yaliyopitishwa.


“Tanzania inathamini ushiriki wa wajumbe wote na mchango wa wadau mbalimbali waliofanikisha mkutano huo, huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake unaoendelea kuiweka Tanzania katika nafasi ya kuhimiza amani, mazungumzo, ushirikiano wa kikanda na maendeleo jumuishi.”


Zungu pia amemshukuru Makamu wa Rais,Deogratius Ndejembi aliyemwakilisha Rais Samia katika ufunguzi wa mkutano huo, akisema Serikali imeonesha dhamira ya kuimarisha ushiriki wa wanawake katika michakato ya amani na usalama kupitia Mpango wa Kwanza wa Taifa wa Wanawake, Amani na Usalama wa mwaka 2025–2029.


Kwa upande wake, Katibu mkuu(ICGLR) Balozi Dkt. Deo Mwapinga, amesema matokeo ya mkutano huo kufuatiwa na hatua za utekelezaji pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa uratibu na ufuatiliaji wa maendeleo ya maazimio yaliyokubaliwa.


“Mfumo huo utasaidia kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama, kufuatilia utekelezaji na kuhakikisha Mpango wa Kikanda wa Wanawake, Amani na Usalama wa mwaka 2027–2031 unatekelezwa kwa ufanisi na uratibu unaofaa,” amesema Balozi Mwapinga


Amesema mkutano huo umepitisha Azimio la Dar es Salaam linalozitaka nchi wanachama kuimarisha sheria na mifumo ya kitaasisi inayowezesha wanawake kupata uwakilishi sawa katika mabunge, serikali na nafasi za uongozi wa vyama vya siasa.


Aidha, azimio hilo pia linahimiza kuongezwa kwa ushiriki wa wanawake katika majadiliano ya amani na timu za upatanishi, kuzuia ukatili dhidi ya wanawake katika siasa, pamoja na kuhakikisha wanaoshiriki katika michakato ya amani wanalindwa dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.


Mwapinga amesema wajumbe wamekubaliana pia kuimarisha usimamizi wa rasilimali za asili kwa kuzingatia usawa wa kijinsia, kupambana na unyonyaji haramu wa rasilimali unaochochea migogoro na kuhakikisha wanawake wanapata sehemu stahiki ya manufaa yatokanayo na rasilimali hizo.


Aidha, alisema azimio hilo limeweka msisitizo katika kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia upatikanaji wa mikopo, ardhi, masoko, biashara za mipakani na elimu ya fedha na teknolojia, huku likitaka kulindwa kwa wanawake na wasichana wakimbizi na waliolazimika kuyahama makazi yao kutokana na migogoro na mabadiliko ya tabianchi.


“Azimio hilo limeitaka Sekretarieti ya ICGLR kufuatilia utekelezaji wake na kuwasilisha taarifa katika kikao kijacho cha kawaida cha Bunge la Umoja huo, huku likihimiza viongozi wa kikanda kulifikisha kwa wakuu wa nchi na serikali, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa,” alisema


Wakati huo huo Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Saada Mkuya, alisema Serikali inaichukulia ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama kuwa sehemu muhimu ya malengo mapana ya maendeleo ya Taifa, kwa kuwa uwezeshaji wa wanawake ni msingi wa kujenga familia imara na jamii zenye ustahimilivu.


Dkt. Mkuya amesema dhamira hiyo inatekelezwa kupitia Mpango wa Kwanza wa Taifa wa Wanawake, Amani na Usalama wa mwaka 2025–2029 uliozinduliwa Agosti 2025, ambao unalenga kuunganisha taasisi za Serikali na wadau wengine katika kuhakikisha ajenda hiyo inatekelezwa katika ngazi zote.


Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa ICGLR kutekeleza Azimio la Dar es Salaam na Mpango wa Pili wa Kikanda wa Wanawake, Amani na Usalama wa mwaka 2026–2030,


Aidha ametoa mwito kwa nchi hizo kudumisha mshikamano na kugeuza makubaliano yaliyofikiwa kuwa vitendo vitakavyoleta amani, usalama na maendeleo katika ukanda wa Maziwa Makuu.


Pia amesema uwezeshaji wa wanawake na usawa wa kijinsia ni nguzo muhimu katika kujenga familia imara, jamii zenye ustahimilivu na taifa lenye ustawi.

“Suala la usawa wa kijinsia halipaswi kuachiwa taasisi zinazoshughulikia masuala ya wanawake na jinsia pekee, bali linahitaji dhamira na ushiriki wa pamoja wa taasisi zote za serikali, jamii na wadau wa maendeleo.


“Dhamira hiyo inaakisiwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na ajenda ya kitaifa ya masuala ya jinsia, zinazolenga kuhakikisha wanawake, wanaume, wasichana na wavulana wanapata fursa sawa za kushiriki na kuchangia katika maendeleo ya taifa.”


Alitaja Mpango wa Tatu wa Kitaifa wa Wanawake, Amani na Usalama wa mwaka 2025–2029, uliozinduliwa Agosti 2025, kuwa nyenzo muhimu ya kuratibu juhudi za taasisi na wadau mbalimbali katika kuendeleza ajenda hiyo, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha unatekelezwa kwa ufanisi katika ngazi zote.


Akitoa salamu za shukrani katika mkutano huo Naibu Spika wa Bunge la Taifa la Zambia, Malungo Chisangano, amesema mkutano huo wa siku nne umewezesha wabunge, viongozi wa serikali, taasisi za kikanda, Umoja wa Mataifa, mashirika ya kiraia na vijana kujadili kwa pamoja nafasi ya wanawake katika kuimarisha amani na kuendeleza ustawi wa eneo la Maziwa Makuu.


Ameongeza majadiliano yaliyofanyika yametoa fursa ya kuhamisha msisitizo kutoka kwenye ahadi za kisera na kuelekeza nguvu katika hatua za vitendo, ikiwemo utungaji wa sheria, utoaji wa fedha kupitia bajeti na usimamizi wa utekelezaji wa sera na mipango ya serikali.


Chisangano amesema Azimio la Dar es Salaam na Mpango wa Kikanda wa Utekelezaji vinapaswa kutumika kama mwongozo kwa mabunge ya nchi wanachama katika kuhakikisha masuala ya Wanawake, Amani na Usalama yanaingizwa katika sheria, sera na mifumo ya usimamizi wa serikali.


Amewataka maspika wa mabunge na wakuu wa ujumbe wa nchi wanachama kuhakikisha maazimio ya mkutano huo yanatekelezwa katika nchi zao, akisisitiza kuwa ushiriki wa wanawake katika ujenzi wa amani na maendeleo si jukumu la wanawake pekee, bali ni kipaumbele kinachopaswa kupewa uzito na mabunge pamoja na taasisi zote za kitaifa.





Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MWENGE WA UHURU WAMURIKA MIRADI YA MAENDELEO JIMBO LA KWELA

MAELFU WAFURIKA TIKTOK LIVE YA DHARURA YA WAZIRI GWAJIMA KUHUSU CHANGAMOTO ZA WANAUME KWENYE NDOA

SERIKALI ITAENDEA KUHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI- LONDO

NMB, UDSM waendeleza ushirikiano wa kukuza vipaji