TANZANIA MWENYEJI WA MKUTANO WA TATU WA IPCC JIJINI ARUSHA


NA MWANDISHI WETU

TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Tatu wa Wataalamu wa Kundi la Kwanza la Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), utakaofanyika kuanzia Novemba 2 hadi 6, 2026, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha PAPU jijini Arusha.

Mkutano huo, unaotarajiwa kuwakutanisha washiriki takribani 300 kutoka sehemu mbalimbali duniani, ni sehemu ya maandalizi ya Taarifa ya Saba ya Tathmini ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (AR7). 


Akizungumzia umuhimu wa mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa IPCC, Dkt. Ladislaus Chang’a, alisema kuwa mwenyeji wa mkutano huo ni fursa muhimu kwa Tanzania kuonesha mchango wake katika sayansi ya hali ya hewa na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.


Alisema mkutano huo pia utaimarisha ushirikiano kati ya wataalamu wa Tanzania, Afrika na mataifa mengine, pamoja na kutoa fursa za kiuchumi kwa watoa huduma mbalimbali nchini.


Mkutano huo utafunguliwa rasmi Novemba 2, 2026, na Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (MB).


Aidha, Novemba 4, 2026, kutakuwa na shughuli maalumu ya uhamasishaji katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika ya Nelson Mandela (NM-AIST) na Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), kwa lengo la kuongeza uelewa wa wadau kuhusu kazi za IPCC na mchakato wa maandalizi ya taarifa za tathmini ya mabadiliko ya tabianchi.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TMA inaendelea kuimarisha mchango wa nchi katika juhudi za kimataifa za kuzalisha na kutumia taarifa sahihi za kisayansi kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.


 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MAELFU WAFURIKA TIKTOK LIVE YA DHARURA YA WAZIRI GWAJIMA KUHUSU CHANGAMOTO ZA WANAUME KWENYE NDOA

MWENGE WA UHURU WAMURIKA MIRADI YA MAENDELEO JIMBO LA KWELA

SERIKALI ITAENDEA KUHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI- LONDO

NMB, UDSM waendeleza ushirikiano wa kukuza vipaji