WAZIRI AKWILAPO ATOA MWANGA MALIPO YA FIDIA UWANJA WA NDEGE MASASI


Na Munir Shemweta, MASASI

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amewatuliza wananchi wa Kijiji cha Mbonde, Wilaya ya Masasi, Mkoa wa Mtwara, wanaodai fidia ya Shilingi bilioni 4.487,944,411.90/= kwa ajili ya kupisha ujenzi na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Masasi, akieleza kuwa malipo hayo yatafanyika kwa awamu tatu kuanzia Novemba 2026.

Dkt. Akwilapo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Masasi Mjini ametoa kauli hiyo leo, Novemba 10, 2026, alipokutana na wananchi hao kijijini Mbonde, kwa lengo la kuwafahamisha hatua iliyofikiwa katika kushughulikia madai yao ya fidia.

Amesema amekuwa akilifuatilia kwa umakini mkubwa suala hilo na kwamba tayari amepata taarifa kutoka Ofisi ya Mlipaji Mkuu wa Serikali kuwa malipo ya fidia kwa wananchi hao yatafanyika kwa awamu tatu.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, awamu ya kwanza ya malipo itakuwa Shilingi bilioni 1.5, inayotarajiwa kufanyika mwezi Novemba 2026, huku awamu ya pili ikiwa ni Shilingi bilioni 1.5 na awamu ya mwisho ya Shilingi bilioni 1.487 ikitarajiwa kulipwa mwezi Januari 2027.

Amesisitiza kuwa, Serikali imelichukulia suala la fidia kwa wananchi hao kwa uzito mkubwa, hivyo kuwataka kuwa na subira wakati taratibu za malipo zikiendelea kukamilishwa.

“Niwaombe wananchi wa Mbonde mnaopisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Masasi muwe na subira wakati mchakato wa malipo ya fidia zenu ukiendelea,” amesema Dkt. Akwilapo.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wanaodai fidia wamemweleza Waziri huyo kuwa wanahitaji uhakika wa malipo yao, wakibainisha kuwa wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu bila kuweza kuendeleza maeneo yao kutokana na kusubiri fidia.

Mmoja wa wananchi hao, Bw. Khamis Bakari, amesema kuchelewa kwa malipo hayo kumewaathiri katika mipango yao ya maendeleo, hivyo kuiomba Serikali kuhakikisha kuwa ahadi ya malipo inatekelezwa.

“Sisi tunaiomba Serikali ituhakikishie malipo yetu ya fidia kwa kuwa tumesubiri kwa muda mrefu na tumeshindwa kufanya maendeleo katika maeneo yetu kama tulivyoelekezwa, tukisubiri malipo, lakini mpaka sasa hatujalipwa,” amesema Bw. Bakari.

Kwa muda mrefu, wananchi wanaopisha ujenzi na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Masasi wamekuwa wakidai kulipwa fidia baada ya maeneo yao kuchukuliwa kwa ajili ya mradi huo, huku kuchelewa kwa malipo hayo kukiwafanya kuwasilisha malalamiko yao katika maeneo mbalimbali.



 


Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MWENGE WA UHURU WAMURIKA MIRADI YA MAENDELEO JIMBO LA KWELA

NMB, UDSM waendeleza ushirikiano wa kukuza vipaji

SERIKALI ITAENDEA KUHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI- LONDO

MAELFU WAFURIKA TIKTOK LIVE YA DHARURA YA WAZIRI GWAJIMA KUHUSU CHANGAMOTO ZA WANAUME KWENYE NDOA