WABUNGE WAPIGWA MSASA UTEKELEZAJI WA BIMA YA AFYA KWA WOTE

 Waziri Mchengerwa awaeleza namna Watanzania watakavyonufaika na mpango huo

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

‎WAZIRI wa Afya, Mohammed Mchengerwa, amewajengea Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uelewa kuhusu utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, unaolenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za matibabu bila vikwazo vya kifedha.

‎Mchengerwa alifungua semina maalumu kwa Wabunge iliyofanyika Novemba 5, 2026 katika Ukumbi wa Pius Msekwa, jijini Dodoma, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Bunge, Cecilia Pareso.

‎Semina hiyo ililenga kuwapa Wabunge uelewa mpana kuhusu utekelezaji wa mpango huo, utaratibu wa kujiunga, makundi yatakayofaidika na namna Serikali inavyosimamia upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.

‎Baadhi ya waliowasilisha mada katika semina hiyo ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya pamoja na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

‎Utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Na. 13 ya mwaka 2023, ambayo imeweka msingi wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa kuzingatia uwezo wao wa kiuchumi.

‎Chini ya mpango huo, wananchi wenye uwezo wanatarajiwa kuchangia gharama za bima, huku Serikali ikiwasaidia wale wasio na uwezo ili nao waweze kupata huduma za matibabu.

‎MAKUNDI MAALUM KUNUFAIKA

‎Katika utekelezaji wa mpango huo, makundi maalum yanapewa kipaumbele, yakiwemo wazee, wajawazito, watoto, watu wenye mahitaji maalum pamoja na kaya maskini zinazotambuliwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

‎Aidha, usajili unafanyika kupitia vifurushi mbalimbali vya bima vinavyolenga kukidhi mahitaji ya watu binafsi, kaya na makundi maalum, vikiwemo Umoja Afya na Toto Afya.

‎Kwa upande wa wageni wanaoingia nchini na kukaa kwa zaidi ya siku 30 bila kuwa na bima ya afya inayotambulika, wanatakiwa kuwa na bima itakayowawezesha kupata huduma za matibabu wanapozihitaji.

‎Usimamizi wa sekta ya bima unafanywa kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), huku Serikali ikiendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na huduma bora katika vituo vya afya.

‎NAMNA YA KUJIUNGA NA BIMA

‎Wananchi wanaweza kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote kupitia mfumo wa kidijitali wa NHIF au kwa kutembelea ofisi za mfuko huo zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini.

‎Utaratibu wa usajili unamwezesha mtu kujiunga binafsi, kupitia kaya au kundi maalum, kwa kujaza taarifa zinazohitajika na kuchagua kifurushi kinachoendana na mahitaji yake.

‎Katika usajili wa mtandaoni, mwombaji anatakiwa kuwa na namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA), huku watoto wakitumia taarifa za cheti cha kuzaliwa kwa ajili ya utambuzi.

‎Baada ya kuingiza taarifa hizo, mwombaji huchagua kifurushi anachohitaji, kisha hujaza taarifa za wategemezi wake endapo anajiunga kupitia kifurushi cha kaya.

‎Miongoni mwa vifurushi vinavyotolewa ni Kifurushi cha Jamii/Kaya kinachotajwa kuwa na gharama ya Sh 150,000 kwa mwaka kwa kaya yenye watu wasiozidi sita, pamoja na Ngorongoro Afya na Serengeti Afya.

‎Baada ya kukamilisha usajili, mwombaji hupatiwa namba ya malipo (Control Number) inayomwezesha kulipia gharama husika kupitia benki au mitandao ya simu inayotambuliwa na mfumo.

‎WANANCHI KUZINGATIA MUDA WA KUSUBIRI

‎Wananchi wanaotaka kujiunga wanashauriwa kuzingatia masharti ya kila kifurushi, ikiwemo muda wa kusubiri kabla ya kuanza kutumia huduma za matibabu.

‎Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, muda huo unaweza kuwa kati ya siku 30 hadi 90 kutegemea aina ya kifurushi kilichochaguliwa.

‎Aidha, mfumo wa NHIF umeelekezwa zaidi katika matumizi ya vitambulisho vya kidijitali, ambapo wanachama wanaweza kutumia taarifa za uanachama au kitambulisho cha NIDA kupata huduma badala ya kutegemea kadi ngumu pekee.

‎Kupitia mpango huo, Serikali inalenga kupanua wigo wa wananchi wanaopata huduma za afya, kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa kaya na kuimarisha ustawi wa jamii.











‎

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MWENGE WA UHURU WAMURIKA MIRADI YA MAENDELEO JIMBO LA KWELA

MAELFU WAFURIKA TIKTOK LIVE YA DHARURA YA WAZIRI GWAJIMA KUHUSU CHANGAMOTO ZA WANAUME KWENYE NDOA

SERIKALI ITAENDEA KUHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI- LONDO

NMB, UDSM waendeleza ushirikiano wa kukuza vipaji