NA MWANDISHI WETU
SHIRIKA la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF), limewataka waandishi wa habari kuweka mkazo katika habari za uhifadhi na mazingira na uchumi wa buluu.
Hayo yamesemwa na Ofisa Program Mwandamizi wa WWF, Happy Minja katika mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari za mazingira yaliyofanyika mkoani Morogoro.
Mafunzo hayo yalishirikisha waandishi kutoka vyombo mbalimbali kwa uratibu wa WWF na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).
Minja amesema uhifadhi wa mazingira ni nguzo muhimu katika kuchochea undelevu wa sekta nyingi, hivyo wameamua kutumia kundi hili la waandishi kusukuma ajenda hiyo.
"Sisi kama WWF tunatamani waandishi wa habari waweke mkazo kwenye masuala ya uhifadhi kwa ujumla, kwa sababu uhifadhi na mazingira ni kila kitu, uhai wetu sisi unategemeana na mazingira," amesema.
Ofisa huyo amesema iwapo waandishi wa habari watapaza sauti serikali itachukua hatua na kulifanya taifa kuwa salama.
Minja amesema WWF imechagua kundi la waandishi kwa kuwa wanaamini ni nguzo muhimu katika kuhabarisha na kuelemisha jamii kwenye eneo la uhifadhi, mazingira, uchumi wa buluu na uwekezaji kwenye eneo hilo.
"Tunapowajengea waandishi uwezo, tunaamini wao watatumia elimu yao kuelimisha taifa na jamii kwa ujumla," amesema.
Minja amesema mafunzo haya ni ya nne, ambapo walianza mwaka 2022, 2023, 2025 na 2026 na wameona mabadiliko makubwa kwenye uhifadhi na mazingira.
Ofisa huyo amesema WWF inajivunia kutumia kundi la waandishi kwani limekuwa likiibua changamoto na wao kuzifanyia kazi kwa usahihi.
Mtaalam wa Uhifadhi na Maliasili, Allen Mgaza amesema kinachofanywa na WWF na JET ni muhimu ili kuhakikisha taarifa sahihi za eneo la uhifadhi na mazingira zinatolewa.
Mgaza ameshauri watekelezaji wa miradi kushirikisha waandishi wa habari kuanzia mwanzo wa mradi ili waweze kuandika habari kwa ufasaha.
"Nadhani kuna haja ya watekelezaji wa miradi kubadilika kwa kushirikisha kundi la wanahabari tangu mwanzo na sio kuja kuripoti matokeo au changamoto," amesema
Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo amesema WWF imekuwa na mchango mkubwa kwenye eneo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari za mazingira na uhifadhi.
Amesema mafunzo hayo yanafanyika kwa mara ya nne hali ambayo inaongeza uelewa na weledi kwa kundi hilo muhimu kwenye kutoa elimu kwa jamii.
"Mafunzo haya ya awamu ya nne yamejikita katika eneo la uchumi wa buluu na uendelevu katika uhifadhi na tumeona mafanikio makubwa tangu tuanze hii program," amesema.
Amesema JET kwa kushirikiana na wadau wengine imeweza kupeleka wanachama wake kwenye maeneo ambayo uhifadhi unafanyika ikiwemo mkoani Tanga kuangalia nyasi bahari ambazo ni muhimu kuhifadhi bahari, wakulima wa mwani na mengine.
Chikomo amesema awali habari za uhifadhi na mazingira zilikuwa haziandikwi kwa kiwango cha kuridhisha ila kwa sasa hali ni nzuri.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Shoroba katika Taasisi ya Kuendeleza Shoroba za Kilimo Tanzania (AGCOT), John Banga amesema wakitoa elimu kwa wakulima wanaweza kutumia mbinu endelevu kwenye sekta ya kilimo.
"Vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuhamasisha kilimo endelevu kinachotunza mazingira na kutafuta masoko ya kisasa na kufikia adhma ya taifa ya uchumi wa buluu na kijani," amesema.
Banga amesema kilimo na mazingira ni pacha kwa kuwa vinategemea hali ya mvua na wadudu ambao wababoresha ardhi kuwa endelevu.


.jpg)
Comments