CHAMA CHA WAHANDISI WASHAURI KUSHEREHEKEA MIAKA 25.

NA VERONICA KAZIMOTO – MAELEZO
DAR ES SALAAM.
Chama cha Wahandisi Washauri Tanzania (ACET), kinatarajia kusherehekea Jubilii ya  miaka 25 tangu kusajiliwa kwake mwaka 1985. Sherehe hiyo itafanyika tarehe 27 Januari, 2011 katika ukumbi wa Karimjee na mgeni rasmi anatazamiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Peter Pinda.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, mwenyekiti wa chama hicho Mhandisi Mwesigwa Kamulali amesema wajumbe wapatao 200 wanategemewa kushiriki katika Jubilii hiyo ikiwa ni pamoja na wageni kutoka nje ya nchi.
“Mpaka sasa wageni 14 kutoka nje ya nchi kama Afrika ya Kusini, Boswana, Zambia, Kenya, Uganda pamoja na nchi za Sudani, Nigeria na Tunisia wamethibitisha kuhudhuria katika Jubilii hii ya miaka 25,” Amesema Kamulali.
Kamulali amefafanua kuwa Jubilii hiyo itaambatana na shughuli kama kuwatambua watu waliokuwa mstali wa mbele kuanzisha chama hicho, kuwatambua wenyeviti wa zamani wa chama hicho, kuwatambua wahandisi washauri wanawake, mihadhara juu ya mada mbalimbali za kitaaluma pamoja na maonyesho ya biashara.
Ameelezea mafanikio ya chama hicho kuwa ni pamoja na kutambuliwa na Serikali, kujenga uwezo wa wahandisi, ushirikiano mzuri wa kikazi kati yake na vyama vingine vya ushauri wa kihandisi ulimwenguni na ukuaji wa uanachama.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo amezitaja changamoto zinazokikabili chama hicho kuwa ni wateja kushindwa kuona tofauti kati ya wahandisi washauri ambao ni wanachama wa ACET na wasio wanachama pamoja na ukosefu wa fursa ya kazi kwa kampuni za kizalendo.
Chama cha Wahandisi Washauri Tanzania ni shirika la hiyari lisilo la kiserikali lenye wanachama 94 na limeanzishwa kwa lengo la kuendeleza ushauri wa kihandisi Tanzania. Madhumuni yake ni kusaidia wanachama kuinua viwango vya taaluma zao ili waweze kutoa huduma za ushauri wa kihandisi kwa ufanisi.
MWISHO.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DK NCHIMBI ATINGA MKOANI KATAVI

BASHASHA LATAWALA NCHIMBI ALIPOLAKIWA NA CHONGOLO SONGWE