MATOKEO KIDATO CHA PILI SI MAZURI

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa
Fredy Azzah 
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imetoa matokeo rasmi ya mtihani wa Kidato cha Pili uliofanyika mwaka 2010, yanayoonyesha  ufaulu umeshuka kwa asilimia 3.52 ikilinganishwa na mwaka 2009.
Katika matokeo hayo, shule za Serikali hazikufanya vizuri  kwa kulinganisha na matokeo ya wastani wa ufaulu kwa shule kumi bora za binafsi. 
Matokeo hayo yaliyotolewa jana na Ofisi ya Habari na kusainiwa na Katibu Mkuu wizara hiyo,  Profesa Hamisi Dihenga, yametaja shule kumi bora za Serikali na nyingine kumi bora zisizo za Serikali.  “Watahiwa 171,395 (38.20%) walishindwa mtihani wakiwamo wasichana 87,593 na wavulana 83,802.
Mwaka 2009 watahiniwa 126,131 (34.6) walishindwa mtihani,” ilifafanua sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza,: “Watahiniwa waliofaulu mtihani ni 227,190  (61.78%), kati yao wasichana ni 113,003 na wavulana ni 164,187,. Idadi ya watahiniwa waliofauli imeshuka kwa asilimia 3.52 ikilinganishwa na mwaka 2009.”
 Wakati shule ya kwanza isiyokuwa ya Serikali ikiwa na wastani asilimia 80, ya kwanza ya Serikali ina wastani wa asilimia 75 ambayo katika matokeo ya jumla inaonekana kushika nafasi ya nane.
Katika mchanganuo huo,  matokeo hayo yanaonyesha shule iliyoshika nafasi ya 10 kwa upande wa Serikali ina wastani wa asilimia 56, huku kwa zile za binafsi ikiwa na wastani wa asilimia 72, wastani ambao kwa shule za Serikali ingetakiwa kuwa ya nafasi ya nne.  Watahiwa 448,640 walijisajili kufanya mtihani huo, ambao kati yao  wasichana ni 215,901 sawa na aslimia 44.15   na wavulana  273,088 sawa na asilimia 55.85.
 “Kumekuwa na ongezeko la watahiniwa 94,481 sawa na asilimia 23.94 ikilinganishwa na mwaka 2009,” iliweka bayana sehemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo,  kati ya watahiniwa waliosajiliwa, walioufanya ni 448,640 sawa na asilimia 91.75 ambao kati yao wasichana ni 200,609 na wavulana 248,031.  “Aidha, watahiniwa 40,337 sawa na asilimia 8.25 hawakufanya mtihani..., kati yao wasichana ni 14,836 na wavulana 25,513, hivyo kumekuwa na ongezeko la watahiniwa 10,802 ambao hawakufanya mtihani ikilinganishwa na mwaka 2009,” ilieleza taarifa hiyo.
 Kwa mujibu wa matokeo hayo, watahiniwa waliofaulu kwa kiwango cha daraja A, B na C walikuwa 132,587 sawa na asilimia 29.56 huku wale waliofaulu kwa daraja D wakiwa 144,603 sawa na asilimia 32.24.  Sehemu ya taarifa hiyo ilizidi kufafanua kwamba, watahiwa 67 sawa na asilimia 0.01 ya waliofanya mtihani huo, wamefutiwa matokeo yao kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za udanganyifu.
Matokeo hayo yanaonyesha pia, masomo matatu ya kwanza ni Historia, Kemia na Uraia ambao yalikuwa  na wastani wa daraja C, huku masomo matu ya mwisho yakiwa ni Baiolojia, Fizikia na Hisabati, yaliyokuwa na daraja D na F.
Kwa ujumla matokeo hayo, yalionyesha   wastani wa ufaulu wa wanafunzi kitaifa ni asilimia 61.78, ikilinganishwa na asilimia 65.3 ya mwaka 2009.
Pia taarifa hiyo ya wizara ya elimu ilitaja sababu nne za matokeo hayo kuwa mabaya, ambazo ni pamoja na  uhaba na upungufu wa walimu katika shule za sekondari na hasa zile za kata.
“Uhaba au ukosefu wa maabara, maktaba, vifaa vya kufundishia na kujifunzia,” inaweka bayana sababu hizo.    Wizara iliongeza kwamba, sababu ya tatu  ni ukosefu wa makazi bora na stahili ya kujifunzia baadhi ya wanafunzi katika baadhi ya shule za kutwa, ukosefu wa motisha kwa walimu, ilitajwa kama sababu nyingine ya tano ya matokeo hayo kuwa mabaya. 
Kwa upande wa shule za Serikali zilizoshika nafasi ya kumi bora na wastani wake kwenye mabano ni Mzumbe (75), Kibaha (74), Iliboru (74) Tabora Boys (67), Iyunga (66), Msalato (65), Musoma Technical (60), Kilakala (59), Mbeya (59) Makuyuni (59). Kwa shule zisizokuwa za Serikali ziliongozwa na Marian Boys (80), Marian Girls (80), Judi Moshono (79), Queen of Apostles Sem, (78) Feza Boys (76), Thomas M Macrina (76), St Francis 76, Carmel (75), Rosmin (74), Feza Girls (72).
Hata hivyo, shule za kata zinaonekana kushika nafasi za mwisho, ingawa licha ya kuzitaja shule za kumi za mwisho za Serikali na zisizokuwa za serikali, hawakuainisha wastani wa zilizopata kama ilivyofanyika kwa shule kumi bora. 
Kwa mujibu wa matokeo hayo, shule kumi za mwisho za serikali ni Tambani, Mofu, Ighmbwe, Mmulunga, Milina, Mwarusembe, Mamndimkongo, Milola, Ugunda na Kibugumo. Upende wa shule zisizokuwa za Serikali nafasi hizo zinashikiliwa na East Cost, Jumuia, Manka, Pwani, City, Doreta, Kwetu, Geogre Washington, Betty Mitchel, Temeke Muslim.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DK NCHIMBI ATINGA MKOANI KATAVI

BASHASHA LATAWALA NCHIMBI ALIPOLAKIWA NA CHONGOLO SONGWE