UTEUZI WA MTEMVU, KIFUKWE 'STOP'

Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu

na Juma Kasesa wa Tanzania Daima

KATIKA hali inayoashiria zimwi la migogoro kuzidi kuizunguka klabu ya Yanga, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Llyod Nchunga, ameibuka na kudai mkutano wa viongozi wa matawi uliofanyika juzi na kuagiza Kamati ya Utendaji kumwajibisha kwa kukiuka katiba, ulikuwa ni batili.
Kuibuka kwa Nchunga, kumekuja siku moja baada ya wenyeviti hao kumtuhumu Nchunga kwa kukiuka katiba, ambapo alimwandikia barua mmoja ya wajumbe wa bodi ya udhamini wa klabu hiyo Francis Kifukwe atafute watu 10 wenye uwezo wa kutoa sh milioni 50 ili kupata sh mil. 500 kwa ajili kuunda kampuni itakayokuwa ikiuza vifaa vya michezo vya Yanga, bila kuishirikisha Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo.
Tuhuma nyingine zilizoelekezwa kwa mwenyekiti huyo, ilikuwa ni uteuzi wa Mbunge wa Temeke, Abass Mtemvu, kuwa miongoni mwa wadhamini wa klabu hiyo, bila ridhaa ya wanachama ambapo jana Nchunga alikiri kuwa kikao cha Kamati ya Utendaji kilichoketi Januari 18 kilipitia uteuzi huo na kubaini kulikuwa na upungufu na hivyo kuamuru kusitishwa kwa suala hilo na mchakato wa kuunda kampuni.
Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya klabu hiyo, jijini Dar es Salaam, Nchunga alisema licha ya mkutano huo kuhudhuriwa na Katibu Mtendaji wa klabu hiyo Lawrence Mwalusako na mjumbe Mohamed Binda, bado ulikuwa ni haramu kwa kuwa ulikiuka katiba kwa kuiamuru Kamati ya Utendaji kumchukulia hatua mwenyekiti, wakati kamati hiyo haiwajibiki kwa wenyeviti wa matawi, isipokuwa kwa mkutano mkuu.
Alisema, mkutano huo ulitokana na chokochoko zinazoenezwa na watu wachache waliozoea kufaidi mali za Yanga bila uhalali wowote na kuuona uongozi wake kuwa msumari wa moto kutokana kukazia suala la ukaguzi wa hesabu za fedha za klabu hiyo zilizotarajiwa ziifikie Yanga, lakini zikaishia mikononi kwa wanachama wachache na aliyekuwa ofisa wa mdhamini wa klabu hiyo.
Nchunga ambaye kitaaluma ni mwanasheria alisema, hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wale watakaothibitika kuhusika na kuitisha mkutano huo usio wa kikatiba ikiwa ni pamoja na kusimamishwa uanachama ndani ya vikao halali.


 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DK NCHIMBI ATINGA MKOANI KATAVI

BASHASHA LATAWALA NCHIMBI ALIPOLAKIWA NA CHONGOLO SONGWE