KAMATI YA BUNGE KUHOJI UFISADI TANESCO

MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Januari Makamba amesema kamati yake italihoji Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), kuhusu upotevu wa mabilioni ya fedha kama ilivyoonyeshwa katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Dar es Salaam jana, Makamba alisema taarifa hiyo ya ufisadi ndani ya Tanesco iliyotolewa na CAG imemsikitisha na kwamba hawezi kukaa kimya.

Taarifa ya CAG iliyoishia Juni 30, 2010 ambayo ilitolewa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge uliomalizika karibuni, ilibaini kuwa Tanesco imeilipa kampuni ya Dowans Sh1.8 bilioni ikiwa ni gharama ya kusafirisha mitambo ya kampuni hiyo kuja nchini kwa ndege badala ya Sh180 milioni.

Matumizi hayo ya ziada yanayokadiriwa kufikia Sh1.4 bilioni yaliingizwa katika akaunti ya Dowans kulipia gharama za usafirishaji mitambo hiyo kimakosa.

CAG alisema hadi sasa, Tanesco imeshindwa kumpelekea ripoti ya matumizi ya fedha hizo alizoziita kuwa ni ufisadi.Jana, Makamba alisema: "CAG ameona madudu ndani ya Tanesco na sisi kama Kamati ya Bunge tunaona ni muhimu Tanesco watoe maelezo. Tutadai watoe maelezo ya kuridhisha kuhusu ufisadi huo."

AlisemaTanesco inashangaza kwa kufanya madudu hayo na kukaa kimya muda mrefu kana kwamba haijui ilichofanya au haina ukaguzi wa hesabu.

Alisema ingawa anatambua kuwa jukumu la kuhoji hesabu ya mashirika ya umma ni la Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma iliyo chini ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kamati yake itadai maelezo hayo kwa kuwa inahusika na shirika hilo.Hata hivyo, katika taarifa yake ya ukaguzi CAG pia ameitaka Tanesco impelekee mchanganuo wa matumizi ya Dola 4,865,000 sawa na Sh6.8 bilioni.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DK NCHIMBI ATINGA MKOANI KATAVI

BASHASHA LATAWALA NCHIMBI ALIPOLAKIWA NA CHONGOLO SONGWE