WAPINZANI WACHUKUENI MAFISADI WATAKAOTOSWA NA CCM

NAPE NNAUYE

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, amesema chama hicho hakitishwi na uwezekano wa vyama vya upinzani kuwachukua makada wake inaotaka kuwatema kwa tuhuma za ufisadi.Msimamo wa Nnauye unakuja kipindi ambacho mpango mkakati huo wa CCM kujivua gamba, ukiwa umeibua mjadala mzito ndani na nje ya chama hicho tawala.

Akizungumza katika kipindi maalumu kilichorushwa na TBC Taifa jana, Nnauye alisema anatangaza zabuni ya bure kwa wapinzani kuwachukua watuhumiwa hao wa ufisadi.

Nnauye ambaye alikuwa akijibu swali kwamba, haoni uamuzi huo wa chama kutema makada wake hao unaweza kuwafanya wakimbilie upinzani, huku akisisitiza: "Tena wakifanya hivyo watakuwa wametusaidia."

Mwanasiasa huyo machachari alifafanua kwamba, CCM ni chama kitukufu kilichojengwa juu ya misingi ya maadili na Baba wa Taifa, marehemu Mwalimu Julius Nyerere, hivyo hakitakumbatia watu wasiokuwa na maadili.

"Ndio maana leo hii kanisa linataka kumfanya Mwalimu Nyerere kuwa mwenye heri, linajua amefanya mambo mengi mazuri. Mwalimu alijenga misingi ya uadilifu ndani ya chama, sasa leo hii watu wasio waadilifu hawawezi kuwa na nafasi,” alisema Nnauye.

Alionyesha tambo akisema: "samaki ana nguvu akiwa ndani ya maji, lakini akishatoka nje hana nguvu. Kwa hiyo hata hawa wanadhani wana nguvu kwa sababu wako ndani ya chama, tukishawatoa mtaona."

Kujivua gamba kwenye jumuiyaNnauye mwana wa kada maarufu wa CCM marehemu Brigedia Jenerali Moses Nnnauye, alisema mchakato wa kujivua gamba hautaishia hapo, kwani ni sawa na kuoga mtu anapaswa kuoga mwili mzima.

Aliweka bayana kwamba, mtu anapooga hugusa viungo mbalimbali ikiwamo mikono na kichwa na kusisitiza: "yapo maamuzi mengi tu tutachukua ikiwamo kugusa jumuiya."

Akitoa mfano, alisema vijana ambao ni karibu asilimia 75 ya wapiga kura wanapaswa kuwekewa mikakati ili waweze kuvutiwa na chama na kama hali ni tofauti, itapaswa kuangaliwa sababu za msingi.

Aliongeza kwamba katika mchakato huo wa kujivua gamba, chama kitashuka ngazi kwa ngazi na hatua kwa hatua hadi kuhakikisha kinarejea katika misingi yake iliyoachwa na waasisi wake.
Kuhusu ukuu wa wilaya Nnauye ambaye amefanya kazi hiyo kwa miezi minane tangu kuteuliwa, alisema anatarajia kukabidhi ofisi wiki ijayo ili aweze kukijenga chama na kukitumikia vizuri.

Alisema hivi sasa watu waliopo kwenye sekretarieti wanapaswa kukitumikia chama peke yake, hata wengine wenye nyadhifa zao watapaswa kuziachia.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DK NCHIMBI ATINGA MKOANI KATAVI

BASHASHA LATAWALA NCHIMBI ALIPOLAKIWA NA CHONGOLO SONGWE