AJIRA ZA UALIMU KUMWAGWA HADHARANI

SERIKALI inatarajia kutoa tamko kuhusu ajira za walimu 25,015 waliohitimu mafunzo ya ngazi mbalimbali katika vyuo vya ualimu nchini wiki ijayo.

Kati ya hao, walimu wa sekondari ni 13,636 wa shahada wakiwa 6,649 na stashahada ni 6,987 na walimu wa shule za msingi ngazi ya cheti ni 11,379.

Hatua hiyo itaondoa hofu kwa wahitimu wa mafunzo ya ualimu ambao wamekaa nyumbani kwa zaidi ya miezi saba wakisubiri ajira, kinyume cha ahadi ya Serikali kwamba wangeajiriwa mara tu baada ya kuhitimu masomo yao.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Kassim Majaliwa alisema jana kuwa mwanzoni mwa wiki ijayo, Serikali itatoa tamko la ajira hizo.

Majaliwa alisema ajira hizo ni kwa ajili ya walimu waliohitimu vyuo mbalimbali vya ualimu kuanzia Mei, 2011 katika ngazi za cheti, stashahada na shahada.

“Napenda kuwataarifu walimu kwamba hakuna mwalimu atakayebaki bila kupata ajira na hatutaki mwalimu afike kituo cha kazi akose mahitaji muhimu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, kwa hiyo mwanzoni mwa wiki ijayo majina yatakuwa kwenye tovuti za Wizara ya Elimu na Tamisemi,” alisema Majaliwa.

Majaliwa alisema tayari utaratibu wa kuwapangia vituo vya kazi walimu hao 25,015 umekamilika na kwamba Wizara ya Fedha imearifiwa ili iweze kupeleka Sh6.2 bilioni katika halmashauri zote nchini ili walimu watakapofika wakute fedha zao tayari.

Alisema hakuna mwalimu atakayebaki bila kuajiriwa kama ilivyokuwa ikielezwa na baadhi ya vyombo vya habari. Alisema sababu za kuchelewesha ajira hizo ni kutaka kukamilisha mahitaji yote ya walimu hao.

Majaliwa alisema Serikali ina nia njema ya kuwapatia ajira walimu wote lakini hawataki kuona mwalimu akifika kazini na kuanza kuteseka kutokana na ukosefu wa mishahara hali ambayo imekuwa ikiwafanya walimu wengi kukimbia vituo vya kazi.

Alisema wakurugenzi wa halmashauri zote wameagizwa kuwapokea na kuwapangia kazi walimu hao watakapofika, baada ya kuwa wamewapatia mahitaji muhimu ili wasitoroke kutokana na hali ngumu ya maisha.

“Hata wakurugenzi wote tumewapa taarifa ya kuwapokea walimu hao bila kuwabughudhi na kuwapatia mahitaji muhimu ya kuanzia maisha ili wawe na moyo wa kufanya kazi kwa ufanisi. Kwa hiyo nawaomba walimu wawe na subira,” alisema Majaliwa.

Baada ya kukaa mitaani kwa takriban miezi saba tangu wahitimu vyuo, walimu hao wamekuwa na hofu ya kukosa ajira ya Serikali na wamekuwa wakiilalamikia Serikali kwa kushindwa kuajiri kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ambayo waliokuwa wakimaliza walikuwa wakiajiriwa mara tu baada ya mafunzo.

Comments

felix mbwanji said…
itasaidia sana maana hali imekuwa ngumu sana.

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA