CHADEMA YATOA MASHARTI KWA JK KUHUSU KATIBA



CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetoa tamko kuhusu mazungumzo yake na Rais Jakaya Kikwete kikisema kwamba kitaridhia mabadiliko ya Katiba Mpya iwapo ataridhia mabadiliko ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba aliyoisaini.

Katika taarifa yake iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari, chama hicho kimeendelea kutishia kususia mchakato huo wa Katiba Mpya kama mapendekezo kilichoyawasilisha Ikulu mwishoni mwa mwaka jana, hayatakubalika.

Novemba 28 na 29 mwaka jana, Chadema kilikabidhi kabrasha la mapendekezo yake kwa Rais kupitia Kamati yake Maalumu kuhusu mchakato wa Katiba Mpya ambayo juzi, ilikutana tena na mkuu huyo wa nchi Ikulu, Dar es Salaam, kujadili hatua zilizofikiwa katika mazungumzo yao ya awali.

Baada ya kikao hicho na Rais, juzi Kamati Kuu (CC) ya Chadema ilikutana jijini Dar es Salaam katika kikao ambacho ajenda yake kuu ilikuwa kupokea taarifa ya kamati hiyo maalumu iliyokutana na Rais Ikulu, ikiongozwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibroad Slaa. 

Jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akisema: “Ushiriki wa Chadema katika mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba utategemea utayari wa Serikali ya Rais Kikwete kufanya mabadiliko ya kimsingi katika sheria hiyo kwa lengo la kujenga muafaka wa kitaifa juu ya mchakato huo.”

Mnyika alifafanua kwamba pamoja na matarajio hayo, CC ya Chadema pia inaona bado ipo haja ya ujumbe wa chama hicho kuendelea kukutana na Rais Kikwete ili kufikia mwafaka wa mchakato huo wa kupata Katiba bora.

“Kamati Kuu imeamua kwamba Kamati Maalumu iendelee kufanya mawasiliano na mashauriano na Rais Kikwete na Serikali kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 inafanyiwa marekebisho ya msingi kabla ya mchakato wa kukusanya maoni,” alisema.

Alisema msimamo huo umechukuliwa baada ya kujadili kwa kina taarifa ya kujulishwa hatua ambazo Serikali imefikia katika maandalizi ya kuifanyia marekebisho sheria hiyo, katika Mkutano wa Sita wa Bunge unaotarajiwa kuanza Jumanne ijayo Mjini Dodoma.

Mnyika alisema wanaendelea kushikilia azimio la CC ya chama hicho la Novemba 20, mwaka jana kwamba, Chadema hakitashiriki kwenye mchakato ulioandaliwa na Serikali.

Azimio hilo lilikusudia kukiamuru chama kiendelee na kampeni za kuwaelimisha wananchi kuhusu; “Ubovu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na juu ya haja ya kuwa na sheria itakayoweka utaratibu bora zaidi wa kuunda Tume Shirikishi ya Katiba kwa lengo la kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa ripoti na rasimu ya Katiba Mpya.”
Chama hicho kinataka liundwe Bunge Maalumu la Katiba na pia uwepo usimamizi wa kura ya maoni, utakaowawezesha wananchi kufanya uamuzi huru na wa haki.

Alisema CC imeendelea kuwaagiza viongozi wote wa chama kama ilivyoelekezwa na Waraka wa Katibu Mkuu Namba 3 wa mwaka 2011, katika ngazi zote kufanya mikutano ya ndani na ya hadhara yenye lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya sheria hiyo na madhara yake kwa mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya.

Alisema mkakati huo wa chama umefafanua: “Kuunganisha umma wa Watanzania kufanya mabadiliko ya msingi kwenye mpango huu wa kupata Katiba Mpya kabla ya mwaka 2014.”

Ahadi ya Rais
Tamko hilo la Chadema limekuja wakati tayari Rais Kikwete ameshatoa ahadi kwamba mchakato wa kupata Katiba Mpya, utaanza hivi karibuni.

Akizungumza na mabalozi kwenye sherehe za mwaka mpya zilizofanyika Ikulu hivi karibuni, Rais Kikwete alisema muda mchache ujao kamati ya kukusanya maoni hayo ya Katiba itakuwa imeingia mitaani. Aliwaahidi kuwa Uchaguzi Mkuu ujao wa 2015, utafanyika chini ya Katiba Mpya.

Kwenye Sherehe za Miaka 50 ya Uhuru, Rais Kikwete alisema pia kwamba mabadiliko ya Katiba anayotarajia kuyasimamia, yamelenga kuleta hamasa ya usimamizi wa maendeleo ya Tanzania katika kipindi cha miaka 50 ijayo.
Jumamosi iliyopita, Rais Kikwete alifanya mazungumzo na ujumbe wa NCCR-Mageuzi na Chadema juu ya maoni yao kuhusu mchakato wa kuandika Katiba hiyo Mpya.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu baada ya mazungumzo hayo ilisema Rais Kikwete alisema licha ya nchi kuwa na Katiba ambayo imelilea vizuri taifa, inahitajika Katiba mpya inayoenda na wakati.

“Katika mazungumzo haya na Vyama vya Siasa, Rais amesisitiza kuwa lengo lake ni kuhakikisha kuwa hatimaye Watanzania wote watakiri kuwa Katiba Mpya ni yao wote na hatimaye ifikapo mwaka 2015 nchi iweze kufanya uchaguzi wake na Katiba Mpya” ilifafanua sehemu ya taarifa hiyo.


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*