Kagashe: Nuru ang'avu iliyozima ghafla

Mkinga Mkinga
Ni saa 3:38 usiku, siku ya Jumamosi (juzi) nikiwa najiandaa kuingia kumjulia hali kaka yangu, Jerome Kamugisha, ambaye amelazwa Hospitali ya Dar Group, napokea ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu yangu ya mkononi unaosomeka ‘Kagashe is dead’.

Ujumbe huo ulikuwa unatoka kwa mmoja wa marafiki zangu ambao pia ni rafiki wakubwa wa marehemu Beatus Kagashe, ambaye nimemfahamu kwa zaidi ya miaka minne iliyopita kama rafiki mkubwa na mfanyakazi mwenzangu katika gazeti dada la The Citizen.

Punde tu, napokea simu kutoka kwa ndugu wa marehemu ambaye alikuwa akiongea kwa kugugumia tena kwa Lugha ya Kihaya, akisema: “Kagashe titukinawe…yatuluga omumikono.” Akimaanisha Kagashe hatuko naye tena.

Katika siku ambazo nilipata wakati mgumu kupokea taarifa za msiba mzito, ilikuwa ni siku ya Jumamosi usiku, tena nikiwa siko katika furaha maana nilikuwa pia hospitali kumjulia hali kaka yangu ambaye sikupenda ajue kinachoendelea, maana pia anamfahamu marehemu kama mmoja wa rafiki zangu wakubwa.

Baada ya taarifa hizo ninapiga hatua kadhaa kurudi nyuma, mwili ukiwa mlegevu tena nikiwa siamini kama rafiki yangu kipenzi siko naye tena duniani. Huku mwili ukikosa nguvu, taratibu machozi yalianza kunilengalenga, sikuweza kijizuia kufuta machozi.

Katika hali ya taharuki, ninachukua simu yangu ya kiganjani naanza kuwapigia baadhi ya wafanyakazi wenzangu, kwa kweli kilikuwa ni kilio kikubwa maana simu ilipokuwa ikipokelewa ni sauti nzito zenye miguno ndizo zilizokuwa zikisikika. Tulifahamu kwamba Kagashe anaumwa kansa ya damu, lakini hatukuwa tunadhani kwamba Mungu angemchukua mapema namna hii.

Hakika! Binadamu hatuwezi kuhoji utukufu wa Mungu, maana yeye ndiye alimuumba Beatus Rwegasira Kagashe na kumkutanisha nasi, katika maneno ambayo pengine huonekana kama hayana maana kwa mfiwa ni pale tunaposema ‘sisi tulimpenda, lakini Mungu kampenda zaidi Kagashe’.

Katika akili ya ubinadamu, unaweza kujiuliza mbona Mwenyezi Mungu kamchukua Kagashe akiwa katika umri mdogo sana wa miaka 31? Hapana. Ninajipa moyo kwamba Mungu ni bwana wa mavuno, hufanya hivyo katika muda wowote ambao yeye anataka.

Maradhi
Kagashe alianza kuugua Septemba na kulazwa Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam, lakini kabla hajaenda hospitali na hatimaye kulazwa alikuwa akitembea upande, katika hali ya mzaha nikamwambia ‘vipi umepigwa na source’ maana ilikuwa ni jioni baada ya kumaliza kazi za kila siku.

Ndipo aliponiambia kwamba anaumwa sana ubavu mmoja na anasikia kama tumbo linawaka moto kuongeza kuwa, alishindwa kula mchana maana akila anatapika, aliniahidi kesho yake kwenda hospitali uchunguzi zaidi.

Alipofika katika Hospitali ya Aga Khan kwa mara ya kwanza, ikawa kama vile sasa ndiyo amefungua maisha yake mapya ya changamoto za maradhi, maana aliniambia amelazwa na hali yake ilikuwa mbaya sana.

Pamoja na kuugua saratani ya damu ambayo kwa kweli ulikuwa huhitaji kuwa na Shahada ya Uzamivu (PhD) kujua Kagashe alikuwa katika mateso na maumivu makali, lakini aliyavumilia tena wakati mwingine yeye akiwa anawapa faraja baadhi ya marafiki waliofika kumjulia hali, huku akionyesha tabasamu muda wote na maneno ya kufariji.

Baada ya kulazwa kwa wiki mbili, lilianza tatizo la kupungukiwa damu, nakumbuka ilikuwa ni Jumamosi nikiwa nyumbani nimepumzika nikapigiwa simu na mmoja wa marafiki, Florence Mugarula, akisema Kagashe anahitaji kuchangiwa damu: Naomba tumsaidie.

Bila kusita, nilikimbia haraka Aga Khan na kutoa damu ambayo kwangu inaacha alama na maana kubwa sana, maana niliweza kumchangia damu nyingi tena nikabaki na alama mkononi kwangu, kumbe nilikuwa ninafumbata maji kwenye viganja.

Mpaka mauti yanamkuta walau alikuwa amekutana na wataalamu wa kitabibu wa kila aina kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Aga Khan na baadaye Taasisi ya Saratani Ocean Road. Lakini ni nani anaweza kupingana na maneno ya maandiko matakatifu kwamba: Sisi ni mavumbi na mavumbini tutarudi.

Elimu yake
Marehemu alisoma Shule ya Msingi Rumuli, alipata elimu ya Sekondari Ihungo, mkoani Kagera hadi mwaka 2000 kabla ya kujiunga na Sekondari ya Mpwapwa, mkoani Dodoma kwa masomo ya kidato cha tano na baadaye mwaka 2003 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (IJMC).

Mwaka 2007, Kagashe alijiunga na Mwananchi Communications Limited, kupitia mpango wa kampuni hiyo wa kutafuta vipaji kutoka kwenye taasisi za elimu ya juu.

Marehemu Kagashe ameacha mke, Doroster Kagashe na mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja, Emmanuel Mujuni Kagashe.

Bwana ametoa, bwana ametwaa jina la bwana lihimidiwe.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA