TUKIO la kuuaga mwili wa askari aliyewaua ndugu zake wawili na baadaye kujimaliza mwenyewe, Nicodemus Senge jana lilikuwa shubiri kwa waandishi wa habari, baada ya polisi kuwazuia waandishi wa habari kufika kwenye tukio hilo lililofanyika katika Kambi ya Polisi ya Msimbazi jijini Dar es Salaam.
Polisi hao ambao baadhi walikuwa wamevalia sare, wakati wote walikuwa makini kuwachunguza na kuwatambua waandishi wa habari waliofika kwenye msiba huo kisha kuwafukuza kwa kile kilichoelezwa kuwa wanapotosha ukweli kuhusu tukio hilo.
Mwandishi wa habari hii ni miongoni mwa wanahabari waliofukuzwa na polisi kwenye msiba huo.Baadhi ya polisi walikuwa getini ambako kuliwekwa uzio wa kamba kuonyesha mwisho wa watu kufika.
"Hatutaki kuwaona waandishi hapa, mimi ni askari na nimeshatoa agizo kwamba asiingie mwandishi yeyote mle ndani," alisema askari mmoja wa kike ambaye jina lake halikujulikana mara moja.Baadaye askari huyo alimchukua mwandishi na kumpeleka ofisini kwao ambako ni sehemu ya mapokezi na kumkabidhi kwa askari mwingine ambaye alikuwa amevalia sare.
Baada ya mwandishi kuhojiwa aliwaeleza kwamba alikuwa akifuatilia taarifa za mazishi ya askari huyo.Polisi huyo alimweleza mwandishi akisema, "huwezi kuingia kwenye nyumba ya mtu bila kujua taratibu zake, tafadhali uondoke, ". Jitihada za gazeti hili kuzungumzia na ndugu wa marehemu ziligonga mwamba baada ya ndugu wote kwa nyakati tofauti kugoma.
“Sitaki kuongea na mwandishi yeyote na hakuna ruhusa ya kuwaruhusu waandishi kuingia hapa kufanya mahojiano na wafiwa, nilikwisha sema wazuiliwe mlangoni iweje wewe uje huku? ”alisema mmoja wa ndugu hao.
Hata hivyo taarifa zilizopatikana msibani hapo zilieleza kuwa mwili wa polisi huyo Nicodemus Senge ungeagwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na baadaye kusafirishwa kwenda kijijini kwake Iyambi wilayani Iramba kwa mazishi.
Awali Ofisa wa Polisi Wilaya ya Kinondoni anayefanya kazi katika Kituo cha Magomeni, Omari Chambo alisema kituo kimempoteza mfanyakazi aliyekuwa anajituma katika utendaji wake , na kusema kuwa saa chache kabla ya kutoka kwa uhai wake alikuwa kazini.
“Kifo cha Nicodemus Senge kimetuhuzunisha kwa kuwa hakuna aliyekuwa anajua kama lingetokea jambo kama hilo, ni saa chache tu yaliyopita kabla ya kifo chake alikuwa kazini” alisema Kamanda Mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela aliiomba familia ya marehemu iwe na amani na moyo wa subira kwa jambo liliojitokeza , kwani Mungu ndiye aliyempenda zaidi.
Comments