Atosha Kissava naye kushiriki Tamasha la Pasaka
TAMASHA la Pasaka linalofanyika kila mwaka kwa kuandaliwa na Kampuni ya Msama Promotions ya Dar es Salaam, linazidi kupanuliwa wigo mwaka huu kwa kushirikisha wasanii nguli. Akizungumza na Jambo Leo, Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama alisema mwimbaji Atosha Kissava kutoka Mkoa wa Iringa amekuwa wa tatu kuthibitisha kushiriki tamasha hilo. "Kissava ambaye ana kundi lake la muziki wa injili, anakuwa mshiriki wa tatu kuthibitisha kushiriki tamasha la Pasaka baada ya Upendo Kilahiro na Upendo Nkone," alisema Msama. Tamasha hilo linatarajiwa kurindima Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Aprili 8 mwaka huu na pia litafanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Aprili 9 mwaka huu. Kissava hivi sasa anatamba na albamu ya Nainua Macho Yangu Juu yenye nyimbo za Alpha na Omega, Unaweza, Nifanane na Wewe, Nibariki na Mimi, Kwake Yesu, Njooni Njooni, Yatima na Nainua Macho uliobeba jina la albamu. "Tunaboresha mambo mengi kuliko miaka iliyopita, waimbaji mwaka huu watakuwa wachache kiasi wakiwamo wa kutoka mataifa mengine ya Afrika... hiyo yote tumefanya ili kukidhi matakwa ya wapenzi wa muziki wa injili. "Mbali na Tanzania, pia tutakuwa na waimbiaji kutoka Kenya, Uganda, Zambia, Afrika Kusini, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika tamasha hilo la nyimbo za injili za kumsifu Mungu. "Mwaka jana hatukuandaa tamasha la Krismasi, hivyo nguvu zote tumezielekeza katika tamasha hili la Pasaka... Wapendwa wajiandae kushiriki kwa wingi kwani watashiba kiroho kwa vile kutakuwa na waimbaji wengi wenye hamasa ya kiroho," alisema Msama. Msama aliyechangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa muziki wa injili akiwa mwasisi wa matamasha ya injili nchini, alisema lengo la kuwajumuisha wasanii hao ni kutaka kulifanya tamasha hilo kuwa tofauti na miaka mingine. Alisema tamasha hilo litakuwa na kiingilio cha chini zaidi (kitatangazwa baadaye), ili kila mmoja ahudhurie na kupata baraka kutoka kwa waimbaji hao wanaomsifu Mungu. "Waimbaji wengi maarufu wa muziki wa injili watakuwepo, tumejipanga vizuri kuhakiksha tamasha hili linakuwa gumzo kila mahali," alisema.
Comments