MATOKEO YA UCHAGUZI JIMBO LA UZINI ZANZIBAR YATHIBITISHA MWISHO WA CUF UMEFIKA

Mshindi wa Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Uzini, kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi Mohammed Raza, akiwaonesha waandishi na wananchi cheti cha kuthibitishwa kuwa mshindi wa uchaguzi huo.

MATOKEO ya uchaguzi mdogo wa uwakilishi wa Jimbo la Uzini, Dunga, Wilaya ya Kati, Unguja, uliofanyika Jumapili ya Februari 12, 2012, yametangazwa na Mohammed Raza mgombea kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kuibuka mshindi wa kishindo huku yakituachia mafunzo kibao.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotolewa na msimamizi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Wilaya ya Kati, Mussa Ali Juma, Raza alizoa kura 5,377 akifuatiwa na mgombea wa CHADEMA, Ali Mbarouk Mshimba (281), Salma Hussein Zaral wa CUF (223), Khamis Khatib Vuai wa Tadea (14) na Rashid Yussuf Mchenga wa AFP kura nane.

Wapiga kura waliojiandikisha katika uchaguzi huo walikuwa 8,743, lakini waliojitokeza ni 5,903 na kura zilizoharibika 28, na kwa maana hiyo wapiga kura ambao hawakujitokeza kupiga kura walikuwa 2,852.

Kwangu mimi matokeo hayo yametoa mafunzo, kwanza kutokana na kura nyingi alizopata Raza ni dhahiri kwamba wananchi wa jimbo hilo wamethibitisha kuwa wameridhishwa na utawala wa CCM, hivyo wapinzani waangalie vema sera zao kama wanatamani kulitwaa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu ujao wa 2015.

Pili, na ambalo ni kubwa kabisa ni kwamba, CUF wanapaswa kuketi haraka kujiangalia walipofikia, ni dhahiri mvutano baina ya Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed na Katibu Mkuu wao Maalim Seif Hamad unakimaliza chama hicho na kama hawatajifunza kwa hili, basi tusubiri kuona kinavyosambaratika.

Naamini kwa kulisema hili watu wengi wa CUF hasa upande wa Maalim Seif watanichukia na kukereka na pengine kuniona kama adui kwa kuwa wao wanaamini Maalim Seif ndiye yuko sahihi na Hamad Rashid si kitu na hana athari yoyote ndani ya chama.

Lakini binafsi nimeona bora niseme hili kwa kuwapa huu Muarobaini ili waunywe kwa kuwa ndio utakaowaponya vinginevyo nisipofanya hivyo nitalazimika kuungana na wengine wanaosubiri kuona jinsi chama hiki ambacho awali kilionekana ndicho pekee chenye nguvu katika upinzani Zanzibar na hata Tanzania bara pia kinavyosambaratika.

Sijui ndugu zetu wa CUF wanasubiri alama gani itokee ndipo wakubali kuwa panahitajika suluhu ya haraka baina ya pande zinazohasimiana ndani ya chama hicho, ikiwa kura 223 alizopata Salma Hussein Zaral, zimefunikwa hata na zile za Ali Mbarouk Mshimba wa CHADEMA aliyepata kura 281.

CHADEMA ambayo hakuna aliyekuwa akiitazamia kupata walau robo ya kura achilia mbali kuzifikia kura za CUF, imemaliza ikiwa katika nafasi ya pili na kuipiku CUF.

Sitaki kuamini kuwa CHADEMA kina wanachama wengi kuliko CUF katika jimbo la Uzini, bali ninachokiamini ni kwamba mgogoro baina ya Hamad Rashid Mohamed na Maalim Seif sasa unahitimisha utawala wa CUF katika siasa za upinzani Tanzania Visiwani na Bara pia.

Kwa wale tuliokuwa tukifuatilia kwa karibu majibizano yalivyokuwa ndani ya CUF tangu hali ya kutoelewana baina ya wawili hawa ilipoanza hadi kuvuliwa uanachama kwa Hamad Rashid na washirika wake na jinsi ambavyo baadhi ya wananchama walivyoanza kujiengua, sasa tunathibitisha kuwa mgogoro huo unaathari kubwa.

Wale waliokuwa wakimbeza Hamad Rashid kwa sababu mbalimbali wanazozijua na kumuona Maalim Seif kuwa mtu asiyekosea au kustahili kuonywa, kukumbushwa ndani ya chama hicho, naamini kwa hili watabadili mtizamo wao.

Wakati baadhi ya watu kutoka maeneo mbalimbali ya bara walipoanza kurudisha kadi baada ya Hamad Rashid na wenzake kuvuliwa uanachama, uongozi wa CUF ulijaribu kuwaaminisha watu kwamba hao ni mamluki lakini kwa uchaguzi huu wa Uzini ni wazi wameumbuka.

Kwa hili walilolionyesha wananchi wa Uzini kuacha kumpigia kura mgombea wa CUF badala yake wakaamua kuzipeleka kwa mgombea wa chama kingine cha upinzani cha CHADEMA na kumfanya Ali Mbarouk Mshimba, kumfunika Salma Hussein Zaral wa CUF kinathibitisha hilo.

Lakini pia wananchi wa Uzini wamethibitisha na kutoa funzo kwamba, hakuna chama chenye hati miliki ya kuongoza, kwamba chama chochote kitakachoamua kuwapigania katika kusaka maendeleo yao watakiunga mkono kama walivyofanya kwa CHADEMA.

Aidha, kwa matokeo haya, wametufunza pia kwamba kila chama kinaposimamisha mgombea kihakikishe kuwa ni mtu anayekubalika mbele ya jamii na si kutokana na sababu nyingine zozote zile kwani pasipo kufanya hivyo kitaadhirika.

Pia matokeo hayo yamethibitisha kuwa, kila chama kinapaswa kufanya uchambuzi wa kina kuhusu kukubalika kwake na kwamba si lazima kusimamisha mgombea pale ambapo kinaamini hakina uungwaji mkono wa kutosha.

Sidhani kama viongozi wa chama makini watakuwa tayari kutumia mamilioni ya fedha kumsimamisha mgombea ili tu kuonekana nacho kimeshiriki uchaguzi, wakati mwisho wa siku mgombea anapata kura zisizofika kumi.

Nimalize kwa kukumbushia hoja yangu kwamba uchaguzi huu mdogo wa Uzini umetuthibitishia pasipo shaka kwamba kama CUF hawatachukua tahadhari basi mwisho wao umefika.
Chanzo;Tanzania Daima

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.