MCHAKATO WA MFUMO WA ITIFAKI YA AMANI NA USALAMA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI WAANZA

Mkurugenzi wa Kitengo cha Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kagyabukama Kiliba akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, kuhusu mchakato wa uundwaji wa mfumo wa Itifaki ya Amani na Usalama kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kulia ni Patrick Mwatonoka ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa masuala ya Siasa wa wizara hiyo. (PICHA NA KAMANDA MWAIKENDA)
Waandishi wa habari wakiwa kazini katika mkutano huo.
Mkurugenzi Msaidizi masuala ya Ulinzi na Usalama wa wizara hiyo, Stephen Mbunda, akifafanua jambo wakati wamkutano huo.
Wanahabari wakiwa kazini

Taarifa kamili

Mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika mashariki umeainisha hatua nne za mtangamano ambazo ni Umoja wa Forodha; Soko la Pamoja; Umoja wa Fedha; na Shirikisho la Kisiasa. Hadi sasa Jumuiya imekwisha anzisha hatua mbili za mwanzo na iko katika mazungumzo ya kuanzisha hatua ya tatu.

Shirikisho la Kisiasa.
Summit iliyokutana Nairobi tarehe 28-29 April 2004 iliazimia kuangalia uwezekano wa kuharakisha hatua za Mtangamano za Jumuiya ya Afrika Mashariki ili Shirikisho la Kisiasa liweze kufikiwa katika muda mfupi kadri inavyowezekana. Summit iliunda Kamati ya wataalamu kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Shirikisho la Kisiasa na kuagiza umuhimu wa kuwapa fursa wananchi kutoa maoni yao kwa mujibu wa kifungu cha 7 cha Mkataba kinachotaka wananchi kushirikishwa (People Centred Principle).

Maoni ya wananchi juu ya Shirikisho la Kisiasa.
Kwa upande wa Tanzania timu iliongozwa na Prof. Samwel Wangwe na ripoti ilionyesha kuwa 75% ya wananchi wa Tanzania hawakuafiki kuharakisha uanzishwaji wa Shirikisho la Kisiasa, 20.8% wanataka liharakishwe, na 3.3 hawataki Shirikisho. Aidha wananchi walieleza hofu, kero na changamoto mbali mbali siyo tu kuhusu Shirikisho lakini kuhusu mtangamano mzima.

Dukuduku lililoanishwa ni pamoja na kupotea kwa utaifa (loss of sovereignty); tofauti katika katiba za serikali za nchi wanachama, hasa katika masuala ya demokrasia na utawala bora; nafasi ya wananchi ya kuamua hatima ya mtangamano; na kutokuulewa vizuri na kutokufahamu faida za mtangamano, Suala la Muungano wa Tanzania katika Shirikisho, uwiano wa mgawano wa faida za kiuchumi na kijamii katika Shirikisho/Jumuiya.

Upotoshaji kuhusu msimamo wa Tanzania.
Kumekuwepo na upotoshaji au wa makusudi au kwa kutoelewa msimamo wa Tanzania kuhusu kuharakishwa kwa Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki. Serikali yetu imekuwa ikilaumiwa kuwa inachelewesha kwa makusudi hatua mbali mbali za mtangamano. Lawama hizo hazina msingi kwani nchi yetu inaamini kuwa jumuiya ina faida nyingi kuliko hasara. Faida hizo hazina ubishi na zimeanza kuonekana.

Hata hivyo ambacho kimekuwa kinasisitizwa na serikali yetu ni kuwa mtangamano sharti uende hatua kwa hatua kama ilivyoainishwa kwenye Makataba wa uanzishwaji wa Jumuiya. Kwa msingi huo sharti tuimarishe na kutekeleza kikamilifu Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja; na wakati huo huo tukamilishe majadilano ya uanzishwaji wa Umoja wa Fedha. Hapo ndio tunapoweza kusema tuko tayari kujadiliana jinsi ya kuanzisha shirikisho.

Sambamba na hilo tunakumbuka jinsi jumuiya ya awali ilivyosambaratika mwaka 1977. Si vizuri kurudia makosa ya nyuma vinginevyo jumuiya ya sasa nayo itavunjika.

Aidha serikali yetu lazima ilinde na kutetea maslahi ya wananchi wake katika majadiliano yo yote ya mtangamano. Kama ambavyo nchi nyingine wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki wanavyolinda na kutetea maslahi ya wananchi wao na nchi yetu sharti ifanye hivyo hivyo.

Tofauti kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki
Jumuiya ya Afrika Mashariki ni taasisi ya kiserikali (Inter Governmental Organization) inayoundwa na mataifa matano ya Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda.

Jumuiya hii ilianzishwa mwaka 1999 na makao makuu yake yako Arusha Tanzania. Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki umetaja hatua nne za mtangamano ambazo ni Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja, kisha Sarafu Moja na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.

Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki (Political Federation) ni hatua ya nne na ya mwisho ya mtangamano ambapo katika hatua hii mamlaka kuhusu baadhi ya shughuli zilizokuwa zinafanywa na Serikali zilizopo madarakani huhamishiwa katika dola inayoundwa. Maana yake ni kuwa madaraka hutoweka katika ngazi ya taifa na hivyo kuhamia katika mamlaka ya Shirikisho.

Kwa msingi huo kuna haja ya kutofautisha kati ya Jumuiya na Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki. Shirikisho la Kisiasa haliwezi kuongelewa tofauti na hatua nyingine za mtangamano huo na sharti tutekeleze kwa ukamilifu Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja, kisha Umoja wa Fedha.

Rule of Consensus.
Kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji EAC makubaliano yote lazima yafanyike kwa “Consensus”. Hii maana yake ni kuwa hakuna utaratibu wa kupiga kura bali maamuzi hufikiwa kwa kila mwanachama kukubaliana na wenzake. Hata hivyo katika siku za karibuni kumekuwepo na maoni kutoka kwa baadhi ya watu kuwa kanuni hii ibadilishwe na maamuzi yafanyike kwa kupiga kura.

Msimamo wetu ni kuwa kanuni hii ni muhimu sana kwa kufanikisha mtangamano. Kama maamuzi yatafanyika kwa kupiga kura ni dhahiri mtangamano hautafika mbali kwani hakuna nchi yo yote mwanachama itakayokubali kuburuzwa na wenzake.

Ushirikiano katika Masuala ya Usalama.
Ili kuhakikisha kuwa amani na usalama vinakuwepo katika nchi wanachama, Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na kuongozwa na Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya pia imeandaa Mpango Mkakati wa Amani na Usalama wa Jumuiya “The Strategy for Regional Peace and Security”.
Mpango Mkakati huu uliidhinishwa na Baraza la Mawaziri wa Jumuiya mwezi Oktoba 2006.

Miongoni mwa malengo yake ni:
kuimarisha ubadilishanaji wa taarifa za uhalifu,
kubadilishana tarifa za hali ya usalama,
kubadilishana programu za mafunzo ya usalama,
kuanzisha mfumo wa kuimarisha operesheni za pamoja,
kuimarisha mawasiliano,
kutekeleza Itifaki ya kupambana na madawa haramu ya kulevya,
viongozi wa vyombo vya usalama kutembeleana,
kuanzisha mfumo wa kudhibiti wakimbizi,
kupambana na ugaidi,
kupambana na uharamia,
kupambana na wizi wa mifugo,
kutekeleza mradi wa kudhibiti kusambaa kwa silaha haramu ndogo ndogo na nyepesi,
kuimarisha usalama katika ziwa Victoria, na
kuandaa mfumo wa kushughulikia migogoro katika kanda.

Ili kutekeleza mpango huu kikamilifu, nchi wanachama zimekamilisha majadiliano ya Itifaki ya Amani na Usalama (Protocol on Peace and Security) ambayo ni mtambuka na inahusisha mambo yaliyotajwa hapo juu. Kikubwa ambacho ningependa kukizungumzia kuhusu Itifaki hiyo ni Early Warning Mechanism, CPMR na kupambana na uharamia katika Bahari ya Indi.

Early Warning Mechanism.
Mojawapo ya njia za kuu za kuepuka migogoro na maafa ya ni kung’amua mapema viashiria vyake. Migogoro inaweza kuwa ni ya kijamii, kiuchumi, kisiasa, lakini pia maafa kama njaa, ukame, mafuriko, n.k. yanasababishwa na sababu mbali mbali. Jumuiya imekubaliana kuunda mfumo wa upashanaji habari mapema kama njia ya kuepuka migogoro na maafa. Uundwaji wa mfumo huu ni maandalizi ya utekelezaji wa Itifaki ya Amani na Usalama mara baada ya kukamilisha matakwa ya kisheria kama yalivyoainishwa katika Mkataba wa Uundwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Rasimu ya Mfumo wa Kupashana habari za tahadhari na majanga ulishakamilika. Kwa sasa nchi wanachama zinajadiliana kuhusu viashiria (indicators) zitakazotumika katika mfumo kitaifa na kikanda.

Rasimu ya Mpango wa Kusuluhisha Migogoro kwa Njia ya Amani (Conflict Prevention, Management and Resolution).
Nchi wanachama zimekubaliana na vipengele vyote vilivyomo katika Rasimu hii. Mpango huu ni utekelezaji wa kifungu cha … cha Rasimu ya Itifaki ya Amani na Usalama ya Jumuiaya mara tu itakapoanza kutumika. Hivyo mpango huu unatarajiwa kuanza kutumika mara baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria kwenye Itifaki ya Imani na Usalama.

Mpango huu madhumuni yake makubwa ni kuzuia migogoro (preventive diplomacy) kulipuka na kusababisha vurugu, ghasia na mapigano. Ili kuufanikisha imependekezwa kuwepo na watu wa “heshima” (Eminent Persons) ambao jukumu lao kubwa itakuwa ni kuzuia na kusuluhisha migogoro pale ambapo itatatokea. Aidha mpango huo utaweka taratibu za kusaidia ulinzi wa amani ambapo vikosi vya kijeshi, polisi na kiraia vya kulinda amani vitapelekwa katika nchi husika.

Mpango Mkakati pamoja na Mpango wake wa Utekelezaji wa Nchi za mashariki na Kusini mwa Afrika (ESA) na zile za Bahari ya Hindi (Indian Ocean Rim) wa Kuimarisha Usalama wa Majini (Regional Strategy Against Piracy and for Matitime Security in the ESA-IO Region)

Kumekuwepo na tishio la Usalama linalotokana na uharamia katika baharΓ­ ya Hindi. Moja ya sababu zinazochangia tatizo hili ni kutokuwepo wa serikali dhabiti katika nchini ya Somalia. Ili kukabiliana na tatizo hili Jumuiya ya Kimataifa iliitisha mkutano wa Kanda ya Afrika Mashariki iliyohusisha Jumuiya za EAC, IGAD, COMESA na IOC. Mkutano huo ulizaa Mkakati na Mpango wake wa utekelezaji (Strategy and Action Plan) wenye maeneo matano kama yafuatavyo:
A SomalΓ­ Inland Action Plan intended to address the supply factors that are making piracy attractive;
Transfer, Detention, Prosecution, Imprisoning and national/regional/legal capability
Capacity building for maritime tasks and support function;
Information Coordination
Preventive and cross-cutting national-regional-international measures
Hili ni suala mtambuka lenye kuhitaji kushirikisha wadau wengi zaidi na tunaendelea kulifanyia kazi.

IMETOLEWA NA WIZARA YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU