POPO WASABABISHA WODI KUFUNGWA BUNDA


WODI ya wanaume katika kituo cha Afya Kasahunga, wilayani Bunda, mkoani Mara, imefungwa kutokana na kuharibiwa vibaya na popo.

Hatua hiyo imesababisha wagonjwa wa kiume kulazwa kwenye wodi ya watoto na wazazi.

Kaimu mganga mkuu wa kituo hicho, Dk. Bahati Moses, jana alimwambia mwandishi wa habari hizi kuwa uongozi wa kituo hicho umelazimika kuifunga wodi hiyo ya wanaume baada ya popo kujaa ndani ya wodi na kusababisha dari kuanguka chini.

Dk. Moses alisema kuwa kwa sasa wagonjwa wa kiume wanalazimika kulazwa katika wodi ya watoto na kwamba wanapokuwa wengi zaidi, kuwalaza hata kwenye wodi ya wazazi na wengine kulazwa chini.

Aliongeza kuwa pia majengo mengi katika kituo hicho yamekwishaharibika kutokana na kutokufanyiwa ukarabati kwa kipindi kirefu na kwamba walikwishaandika maombi ya kukarabati kituo hicho tangu mwaka 2009, lakini hadi sasa bado ukarabati haujafanyika na hali inaendelea kuwa mbaya zaidi.

Alisema kituo hicho pia kinakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa madawa, pamoja na maji, ambapo wagonjwa wamekuwa wakilazimika kufuata maji ziwani, ambako kuna umbali wa zaidi ya kilomita mbili.

Aliongeza kuwa pamoja na kuwa na mtambo wa kusukuma maji kutoka katika chanzo cha maji kilichoko katika kijiji cha Nyamitwebili, lakini wamekuwa hawapati maji hayo, kwa kile kinachoelezwa kwamba mabomba yamekwishakatika.

Alisema kuwa kufuatia hali hiyo mazingira ya usafi katika kituo hicho si ya kuridhisha kwani wamekuwa wakideki vyumba kwa kutumia maji kidogo wanayopata kwa kununua kwa watu.

Kuhusu upungufu wa dawa Dk. Moses alisema kuwa utaratibu wa kupata dawa ni baada ya miezi mitatu, lakini hilo limekuwa halizingatiwi, kwani inafikia hata miezi sita bila kuletewa dawa na kwamba zinapoletwa huwa hazikidhi mahitaji.

“Hata hivyo dawa zinakuja kidogo sana, mfano unaweza kuagiza makopo kumi, lakini badala yake unaletewa makopo mawili tu.......tena dawa zingine muhimu haziletwi,” alisema.

Alisema kutokana na upungufu huo wa dawa wagonjwa wamekuwa wakilazimika kuzinunua kwenye maduka ya watu binafsi, huku lawama nyingi zikiwaendea watumishi wa kituo hicho kwamba huenda wao ndio wanaoficha.

Wakati huohuo, watumishi wa kituo hicho wameilalamikia idara ya afya wilayani hapa, kwa kutowapandisha vyeo kwa kipindi kirefu, licha ya kuwa na sifa zinazostahili, ikiwa ni pamoja na kutokuthibitishwa kazini na kutokupewa posho za likizo.

Walisema kuwa uthibitisho kazini kwa mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2007 na kupandishwa vyeo kwa mara ya mwisho ilikuwa ni mwaka 1992.

Mganga mkuu wa wilaya ya Bunda, Dk. Rainer Kapinga, alipoulizwa kuhusu hali hiyo, alisema kuwa kituo hicho hakijakarabatiwa kutokana na kukosekana kwa ruzuku ya maendeleo katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2010/2011, na kwamba sasa wanatumia ruzuku ya kawaida kwa ajili ya kukarabati majengo hayo.

Kuhusu madai ya watumishi wa idara ya afya, Kapinga alisema wamekuwa wakilipwa haki zao zinazostahili, ambapo pia amekanusha kwamba hakuna mtumishi ambaye hajalipwa madai yake, ikiwemo posho ya kujikimu pamoja na nauli.

Naye ofisa utumishi wa halmashauri ya wilaya ya Bunda, Gregory Rugemalira, alisema wamekuwa wakipandisha vyeo watumishi mara kwa mara na kwamba wale ambao hawajapandishwa ni wale ambao hawataki kujiendeleza kielimu, ili waweze kuwa na sifa zinazotakiwa. Chanzo;gazeti la Tanzania Daima.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.